************************
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA WIZI WA MIFUGO.
Mnamo tarehe 22.02.2022 majira ya saa 10:00 asubuhi huko Mbalizi kati, Kata ya Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walifanya msako wa kuwakamata watuhumiwa mbalimbali kwa nia ya kuzuia uhalifu na kufanikiwa kumkamata FADHILI HAKIMU [24] Mkazi wa Horongo aliyekuwa anatuhumiwa kuiba mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi 280,000/= mali ya ALEMAN TAMAELI [71] Mkazi wa Horongo.
Mtuhumiwa aliiba mbuzi hao mnamo tarehe 21.02.2022 huko nyumbani kwa mzee ALEMAN TAMAELI [71] na mara baada ya taarifa kufika Polisi msako ulianza na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye amekiri kuhusika katika tukio hilo. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
KUKAMATWA MTUHUMIWA WA WIZI WA PIKIPIKI.
Mnamo tarehe 22.02.2022 majira ya saa 12:30 mchana huko Ifupa, Kata ya Ilungu, Tarafa ya Tembela, Wilaya na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa katika Misako walimkamata FRANK KAYANGE [35] Mkazi wa Kayuki – Ushirika Tukuyu akiwa na Pikipiki ya wizi yenye namba za usajili MC.560 CPJ aina ya Kinglion, Chasis Na. LTBPK8BG4L2KO1665, Engine Na. KL162FMJ*20J01665 mali ya PAUL EDWARD [30] Mkazi wa Itanchi Uyole.
Mtuhumiwa alikamatwa na kukutwa na Pikipiki hiyo akiwa amebadilisha namba ya usajili na kubandika namba MC.911 CPJ. Pikipiki hiyo imetambuliwa na mmiliki wake. Mahojiano na mtuhumiwa yanaendelea ili kubaini mtandao wa wezi na wanunuzi wa Pikipiki za wizi.
KUKAMATA BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI NA ZILIZOKWEPA USHURU WA FORODHA.
Mnamo tarehe 22.02.2022 majira ya saa 10:00 asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Idara ya Forodha walifanya msako huko Stendi ya Mabasi Lubelele iliyopo Kata ya Kasumulu, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kukamata bidhaa zilizokwepa kulipiwa ushuru wa forodha ambazo ni:-
Sukari mifuko 15 yenye jumla ya Kilogramu 397
Aidha katika msako huo zilikamatwa bidhaa pombe kali zilizopigwa marufuku nchini ambazo ni WIN chupa 20, Rider chupa 12 na Right Choice chupa 04 zenye ujazo wa 200mls kila moja. Msako wa kuwatafuta watuhumiwa unaendelea.