Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, (watatu kulia) akimkabidhi cheti cha pongezi cha taaluma mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Tarangire ya Mjini Babati Mkoani Manyara, Mandela Mselu, kutokana na ufaulu mzuri wa shule yake, wapili kulia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul
***************
Na Mwandishi wetu, Babati
SHULE ya awali na msingi Tarangire ya mchepuo wa kiingereza ya Mjini Babati Mkoani Manyara, imenyakua tuzo tano kwa walimu na tatu za wanafunzi kutokana na ufaulu mzuri.
Wanafunzi watatu na walimu watano wa shule hiyo walipatiwa vyeti mbalimbali vya taaluma vilivyotolewa na Halmashauri ya Mji wa Babati.
Zawadi hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga kwenye siku ya elimu mjini Babati ambapo walimu na wanafunzi hao walishikana mikono na kupongezwa na Kipanga.
Wanafunzi waliopatiwa vyeti ni Helen Gerard, Magreth William na Ridhiwani Said na walimu ni Juma Amma, Peris Samweli, Mandela Mselu, Peter Chami na Hassan Mapande.
Mwalimu mkuu wa shule ya Tarangire, Mandela Mselu amesema shule hiyo ilipata tuzo tatu kutokana na kuwa ni mojawapo ya shule tano zilizofanya vizuri zaidi katika wilaya ya Babati kati ya shule 42.
Mandela amesema shule ya Tarangire ilipata tuzo tatu ambazo ni shule iliyoingia 10 bora, shule isiyokuwa na alama D katika matokeo yake na shule yenye ubora wa taaluma.
Amesema pamoja na tuzo hizo za jumla za shule, walimu wote wanaofundisha masomo darasa la nne na la saba walipewa vyeti vya pongezi kwa kufanya vizuri katika masomo yao yote.
“Mwalimu mkuu wa shule alitunukiwa cheti maalum kwa kuwa kiongozi katika shule inayofanya vizuri na wanafunzi wanne walipewa zawadi kwa kufanya vizuri kiwilaya kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la nne,” amesema.
Mwalimu mkuu wa shule ya awali na msingi Tarangire Mandela amesema siri ya wao kupata vyeti hivyo ni kujituma, ushirikiano wa walimu na wanafunzi na maandalizi mazuri.
Mgeni rasmi wa tukio hilo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amewapongeza walimu na wanafunzi wa shule zote zilizopatiwa vyeti vya ubora kwenye taaluma zao.
“Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya elimu hivi sasa, hivyo jamii inapaswa kutimiza wajibu wao kwa watoto wao nasi tutatimiza yetu kwa wanafunzi,” amesema..