Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam. Februari 22,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea maelezo kutoka kwa washiriki wa maonesho ya bidhaa za madini katika Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam. Februari 22,2022.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungummza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam. Februari 22,2022.Wadau mbalimbali wa Madini wakifuatilia ufunguzi wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam. Februari 22,2022.
*******************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 22 Februari 2022 amefungua Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Serikali imeendelea kuzifanyia kazi na kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya madini ikiwemo ya kuanza kutoa kipaumbele katika utoaji leseni za uchimbaji madini kwa wamiliki wa mashamba katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Bulumbaka Gold Rush.
Aidha amesema kwa sasa upatikanaji wa leseni kwa wawekezaji unafanyika kwa haraka kutoka miaka miwili na zaidi hapo awali hadi kufikia miezi sita.
Makamu wa Rais amesema Serikali imejenga Mitambo ya uyeyushaji na usafishaji dhahabu katika mikoa ya Geita, Mwanza na Dodoma pamoja na kuingia makubaliano na Kampuni ya Tembo Nickel kujenga Mitambo ya uyeyushaji na usafishaji madini ya aina zote, Wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Aidha Makamu wa Rais amezitaka Benki na Taasisi nyingine za Kifedha kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kubuni namna bora zaidi ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wakati Serikali ikiwa inalifanyia kazi suala la kuanzisha Benki maalum ya Madini.
Amesema ni muhimu huduma hizo ziende sambamba na kutoa elimu kwa Wateja hasa kuhusu ubora na usimamizi wa miradi na matumizi adili ya Mikopo inayotolewa.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaasa wawekezaji wakubwa, kuendelea kuboresha uchumi wa wananchi katika maeneo yenye migodi kwa kutoa fursa za ajira katika na kujenga urafiki na jamii zinazowazunguka ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Makamu wa Rais amewahimiza kuzingatia sheria mbalimbali za nchi ikiwemo kulinda mazingira pamoja na kutowatumia watoto katika ajira maeneo ya migodini.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Doto Biteko amesema mkutano huo umekuwa na mafanikio mengi yanayotoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya madini nchini.
Amesema tayari mkutano huo umeleta manufaa ikiwemo kuongeza wawekezaji katika nchi pamoja na kuongezeka kwa kampuni za utafiti wa madini hapa nchini.
Amesema wawekezaji wengi wameendelea kuja nchini kutafuta fursa za uwekezaji kutokana na matokeo ya mkutano huo.
Waziri Biteko amemuhakikishia Makamu wa Rais kwamba Wizara ya Madini itaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika mikutano ya wadau wa sekta ya madini kwa ufanisi mkubwa.
Awali rais wa Wachimbaji wadogo wa madini John Bina ameipongeza serikali kwa hatua mbalimbali za uboreshaji wa sekta ya madini hapa nchin na kueleza kwamba pamoja na mafanikio hayo bado wachimbaji wa wadogo wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji kwa kukosa mikopo nafuu kutoka kwa taasisi za fedha na kuomba serikali kuanzisha mfuko wa uendeshaji wa uchimbaji mdogo ili kuongeza ajira na kupandisha viwango vya ulipaji kodi.