Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari wakifuatilia mada ya umuhimu wa kufanya mazoezi iliyokuwa inatolewa kwenye mafunzo hayo yanayofanyika katika Ukumbi wa Protea jijini Dar es Salaam. Mfunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).
Mkurugenzi Msaidizi huduma za lishe kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Moshi akiwasilisha mada kuhusu lishe bora inavyoweza kuwakinga watu na magonjwa yasiyoambukiza kwa washiriki wa mafunzo ya kujenga uwezo wa kuyafahamu magonjwa hayo ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari . Mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Andwer Swai akitoa mada ya ugonjwa wa kisukari kwa washiriki wa mafunzo ya kuwajenga uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari . Mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika katika Hoteli ya Protea iliyopo jijini Dar es Salaam imeandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).
Washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo yanayofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).
Picha na Henrick Chiwangu
…………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Wanawake nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuzikinga familia zao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuandaa mlo bora kwani magonjwa hayo yanatokana na mtindo mbaya wa maisha ikiwa ni pamoja na kula vyakula bila mpangilio.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Malinyi Mhe. Antipas Mgungusi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuyafahamu magonjwa yasiyoambukiza wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, watu wanaoishi na magonjwa hayo na wahariri wa vyombo vya habari yanayofanyika katika Hoteli ya Protea iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mgungusi alisema mkurugenzi wa masuala ya chakula na lishe katika familia ni mwanamke na kuwataka wanawake katika familia kuchukua majukumu yao ya kuhakikisha familia zinapata chakula bora kisichokuwa na mafuta mengi, sukari nyingi na chumvi nyingi ili kuzikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
“Mara nyingi sisi wanaume tukitoka katika mihangaiko yetu tukifika nyumbani tunakula chakula tulichoandaliwa mezani, hivyo basi kama mama kaandaa chakula hatarishi kwa afya tunakula lakini pia kama kaandaa chakula chenye afya bora tutakula. Hivyo ni vyema wanawake kuwa mstari wa mbele katika kuokoa familia zao na magonjwa haya yasiyoambukiza”, alisema Mhe. Mgungusi.
Mhe. Mgungusi ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza aliwaomba wadau wa maendeleo nchini kuungana kwa pamoja kutafuta mbinu zitakazowezesha magonjwa yasiyoambukiza yanapungua kwani magonjwa hayo hutumia gharama nyingi kuyatibu na kuzifanya familia kubaki maskini.
“Changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza ni kubwa, tumeona watu wengi wanapoteza maisha, lakini pia magonjwa haya yanafahamika kuwa ni magonjwa ambayo tiba zake ni za gharama kubwa. Ni vyema jamii ikatumia njia mbalimbali za kujikinga na magonjwa haya kwani gharama za kujikinga ni ndogo kuliko gharama za matibabu endapo mtu atapata magonjwa haya”, .
“Nikitoka hapa nitachukua jukumu langu la msingi la kuelimisha watu juu ya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo, kansa, kisukari, pumu na selimundu kwani watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa haya hivyo kupelekea wagonjwa kugundulika kuwa na matatizo haya wakiwa katika hatua mbaya”, alisema Mhe. Mgunguzi.
Kwa upande wake Meneja wa elimu ya afya kwa umma na kaimu meneja kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bakari Magarawa aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau binafsi kwa juhudi zao za kupambana na magonjwa hayo.
Magarawa aliwaomba wadau kuendelea kuhamasisha jamii namna inavyoweza kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuanzisha mafunzo mbalimbali yanayotoa elimu katika makundi rika na kuikinga jamii na magonjwa yasiyoambukiza.
“Ni jukumu letu kila mtu kwa wakati wake kupambana na kuipambania jamii iliyotuzunguka ili kwa pamoja tuweze kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakitumia gharama kubwa kuyatibu hivyo kupelekea uchumi wa nchi na uchumi wa familia kutumika katika matibabu badala ya kutumika katika maendeleo mengine”, alisema Magarawa.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo Mhariri Mkuu wa Clouds Media Group na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Joyce Shebe alisema mafunzo ya kuwajengea uwezo aliyoyapata yamemfungua macho na kuona ukubwa wa tatizo hivyo kumpa jukumu kama mwandishi wa habari kuisaidia jamii kutoa taarifa za kuelimisha umma ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Joyce alisema waandishi wa habari wanapaswa kuisaidia jamii ya watanzania ili iweze kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza kwa kutumia vyombo vyao vya habari wataweza kuhamasisha mbinu ambazo zitazuia magonjwa hayo kama kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kula vyakula bora na kufuata mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa hayo.
“Ninaiomba Serikali iwe inatoa takwimu za magonjwa haya kwa kutupa nafasi ya kujua ukubwa wa tatizo ili kwa pamoja sisi kupitia vyombo vyetu vya habari tuingie kwenye vita ya kupambana na magonjwa haya na kuikinga jamii yetu na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Joyce.
Naye Mbunge wa Vitu Maalum kutoka Mkoa wa Pwani ambaye pia mjumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua kikuu, madawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza Mhe. Hawa Chakoma aliipongeza Serikali kwa jitihada inayofanya ya kupambana na magonjwa hayo kwa kutenga bajeti inayotumika kununua vifaa tiba, dawa na kuwasaidia wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza.
“Magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakichukua bajeti kubwa ya Serikali katika kuyatibu, ni jukumu letu sasa kupaza sauti zetu ili kuyapunguza ikiwezekana kuyaondoka kabisa magonjwa haya kwani hayahitaji bajeti kuyaondoa bali uhitaji jitihada zetu katika kujikinga nayo”, alisema Mhe. Hawa
Aidha Mhe. Hawa alilipongeza Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) kwa kuwa mstari wa mbele katika kupambana kwa ajili ya kuikinga jamii na magonjwa hayo kwa kutoa mafunzo mbalimbali na kuwafikia wagonjwa ambao tayari wanaishi na magonjwa hayo ili wawe ushuhuda katika jamii kwa kujitokeza na kutoa changamoto mbalimbali wanazopitia.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanayohudhuriwa na washiriki 64 yameandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA).