Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwafuata wafanyabiashara kwenye maeneo yao ya kazi ili kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, hali itakayowajengea ari ya kulipa kodi kwa hiari.
Mhe. Hapi aliyasema hayo wakati timu ya maofisa wa TRA walipomtembelea ofisini kwake kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo imemalizika leo mkoani humo.
Alisema kuwa, kuna baadhi ya nchi wamefikia hatua anayegombea nafasi ya uongozi, historia yake ya ulipaji kodi inafuatiliwa na ikibainika aliwahi kukwepa kulipa kodi anapoteza sifa ya kugombea.
“Naamini kama nchi siku moja tufike mahali ambapo ili ugombee uongozi, historia nzuri ya ulipaji kodi iwe moja ya sifa, iwe fahari kuwa mimi ni mmoja wa walipakodi na ni sehemu ya maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Hapi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara, viongozi wa wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wote kwa ushirikiano walioutoa kwa timu ya maofisa wa TRA waliofanya kampeni hiyo mkoani humo na kufanikisha kuwafikia jumla ya wafanyabiashara 4,014.
“Katika zoezi hili, tumefikia jumla ya wafanyabiashara 4,014 ambapo Wilaya ya Tarime tumefikia wafanyabiashara 2,088, Bunda 1,126 na Musoma mjini tumefikia wafanyabiashara 800,” Alieleza Bw. Kayombo.
Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara Bw. Boniphace Ndengo ameishukuru TRA kwa kutoa elimu mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha mabadiliko ya sheria za kodi kila zinapopitishwa na Bunge.
“Niishukuru Idara ya elimu kwa mlipakodi, kazi mnayoifanya ya kutuelimisha ni kubwa sana. Moja ya eneo ambalo wafanyabishara tumekuwa tukilalamika ni kwamba sheria inapotungwa inaanza kutekelezwa mara moja lakini kwa sasa tunashukuru mnavyokuja kutupatia taarifa mapema ili na sisi tujipange vizuri,” Alisema Bw. Ndengo.
Wafanyabiashara wa Wilaya ya Musoma mkoani humo kwa nyakati tofauti wamesifia kitendo cha TRA kupita mlango kwa mlango kuwapatia elimu na kusema kwamba, wameepushwa na makosa yanayotokana na kutokuwa na uelewa wa masuala ya kodi.
Nyangaro Mseti ni mfanyabiashara wa Musoma mjini ambaye ameeleza kuwa, utaratibu huo unawasaidia kupata muda wa kutosha kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabiri.
Mfanyabiashara mwingine ni Eunice Julius, ambaye alisema awali walikuwa wakiitwa eneo moja kwa ajili ya kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ya kodi, lakini baadhi yao walikuwa hawaendi kwasababu walishindwa kufunga biashara wakihofia kukosa mauzo.
“Sasa mnatufuata na kutufundisha, akija mteja mnasubiri mpaka nimalize kumhudumia kisha mnaendelea, kwakweli utaratibu huu ni mzuri sana maana elimu tunapata na mauzo hayapungui ndiyo maana naomba muendelee tena mje mara kwa mara,” alisema Julius.