NAIBU Waziri wa Wizara ya Habari mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhandisi Andrew Kundo amesema ili Jeshi la polisi likomeshe uhalifu wa kimtandao linatakiwa kuwekeza katika Teknolojia.
Hayo ameyasema leo Februari 21,2022 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya Makosa ya mtandao (CYBERCRIME)kwa wapelelezi na askari wa chumba cha mashtaka(CRO) amesema Mafunzo hayo ni ya muhimu kwa Dunia ya leo ambayo imejawa na uhalifu kwasababu ya ongezeko la wabuni mbinu za uhalifu ni wengi na kila siku wanabuni mbinu mpya za uhalifu.
Amesema Kamati pamoja na mambo mengine ilipendekeza kutoa mafunzo hayo na serikali iliridhia mafunzo hayo ili kumfanya askari kuwa bora kwasababu mhalifu anaweza kuwa bora lakini askari anatakiwa awe bora zaidi.
“Lengo la jeshi letu kuwa la kisasa na linalojibu kiu ya watu katika utekelezaji wa huduma bora hivyo wananchi wanataikwa watambue nini maana ya makosa ya mtandao kupitia sisi kwenye vyombo vya habari mbalimbali nchini,”amesema.
Amesema Mafunzo hayo yanafanyika Morogoro,Dar es Salaam na Dodoma ili kulijengea uwezo jeshi la polisi nchini kuwa imara katika kutatua uhalifu wa kimtandao kupitia Teknolojia.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa mashtaka nchini (DCI),kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi(SACP)Deusdedit Nsimeki,alisema mafunzo hayo kupata uelewa mpana wa sheria ya makosa ya mtandao na kufanya taaluma hiyo katika kumsaidia mwananchi sio kujipatia kipato.
Amesema kumekuwa na malalamiko toka kwa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa na kesi ya kupotelewa na simu zao kulipia gharama kubwa tofauti na simu ambayo imepotea na hivyo kuharibu taswira ya jeshi na taaluma kwa ujumla.
“Mafunzo hayo yatasaidia kuongeza tija na uadilifu katika utendaji kazi wenu ikiwa ninpamoja na kupambana na uhalifu na kupelekea kufanyakazi kwa ushirikiano mkubwa,”amesema.
Kamishna wa Polisi uchunguzi wa kisayansi (CP FB) Shabani Hiki ameishukuru Wizara kwa kulitendea haki jeshi la polisi kwa kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wataalam wa jeshi la polisi kwasababu lawama nyingi za wananchi kwa jeshi hilo yanaanzia katika chumba cha mashtaka hivyo mafunzo hayo yatasaidia kupunguza malalamiko kwa jeshi la polisi Tanzania kwa upande wa mashtaka yote ya uhalifu mtandaoni
Mafunzo ya kukabiliana na makosa ya uhalifu mtandaoni yanaendeshwa katika maeneo tofauti ya Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro, ambapo wataalamu zaidi ya 400 wanapatiwa mafunzo yanayohusu Upelelezi wa Makosa ya Kimtandao, Ubobezi katika Tathmini ya Usalama wa mifumo na Sayansi ya kiuchunguzi katika mitandao, Matumizi ya moduli ya uhalifu mtandao, Uandaaji wa Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka kwa Mashauri ya Kimtandao, sheria za kuzuia uhalifu mtandao pamojua na ujuzi wa uchunguzi na uendeshaji mashtaka.