Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi kituo hicho Diwani wa Bulale (CCM),Deogratius Kabadi, alisema watu wengi walilalamikia tozo ya miamala kwa kutofahamu manufaa yake,hivyo kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Afya Bulale, Watanzania wauone mpango huo ulikuwa na lengo zuri lenye tija na manufaa kwa jamii.
Alimpongeza Rais Samia kwa kutoa fedha za mradi huo pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi Robert Gabriel kwa moyo wa kizalendo wa kushiriki na wananchi kuchimba msingi wa jengo la kituo hicho kisha kunywa nao uji,kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na viongozi wengine mkoani humu na hivyo Rais Samia Suluhu Hassan,hakukosea kumteua kuiongoza Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, alisema Rais Samia anastahili pongezi na kuungwa mkono kwa kuijali Nyamagana na kuipa fedha za miradi ya kimkakati na sekta mbalimbali za umma.
“Mkuu wa Mkoa (Mhandisi Gabriel),matunda ya mradi huu yana mchango wako,watendaji na usimamizi wa fedha zinazotolewa na Serikali ya CCM,tumeanza kujenga barabara za lami,mradi wa maji Butimba wa sh. bilioni zaidi ya 69,Sahwa sh. bilioni 17.89.Pia tumepata sh. milioni 900 za hospitali ya wilaya na vituo vya afya na sh. milioni 400 za zahanati,”alisema
Makilagi alisema wataisimamia miradi hiyo kwa umakini na kuhakikisha chenchi inabaki ambapo fedha za chenchi za kituo cha Afya Bulale,anaamini zitaleta matokeo chanya kwa kununua vifaa bora vya maabara,dawa na vitendanishi.
Naye Mhandisi Gabriel,akizungumza kabla ya kukabidhi kituo hicho,alisema Mwanza inaongoza kwa vifo vya wajawazito na watoto,hivyo kitakuwa mwarobaini wa kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
“Kukamilishwa kwa kituo hiki cha Afya Bulale na wataalamu ni jibu sahihi mwanamke mjawazito hafi na ujauzito pamoja na watoto kwa kukosa huduma.Tuna uhakika changamoto ya mama na mtoto haitachukua muda mrefu,tuhakikishe afya ya mama na mtoto inakuwa salama,”alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa mwaka 2019/20 kulikuwa na vifo vya uzazi 157 ambapo mwaka 2020/21 viliongezeka na kufikia vifo 164 vya watoto wakiwa 669 kwa mwaka 2019/20, mwaka 2020/21 vifo vya watoto vilikuwa 71 na kwa takwimu hizo ujauzito ni ugonjwa na balaa linaloweza kusababisha vifo.
Pia alieleza zaidi wananchi wengi hawatumii huduma za afya ya uzazi tangu mwanzo wa ujauzito hadi kujifungua na kuwataka wakitumie kituo hicho kupata vipimo na ushauri ili wenye matatizo wapate huduma muda wote wa ukuaji wa mimba hadi kujifungua.
“Tusiruhusu tena vifo vya akinamama na watoto wengine,haya yamemsukuma Mh. Rais Samia kuwekeza nguvu kubwa kwenye afya ya msingi ili kuokoa maisha ya watu (wananchi) wake,ametupunguzia changamoto hii tuwe salama na hivyo tuendelee kutumia huduma kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa salama,dawa,vifaa tiba na vitendanishi vya kisasa vyenye ubora vipatikane,”alisistiza.
Mhandisi Gabriel kuhusu chenchi ya fedha sh.milioni 13 iliyookolewa kwenye mradi huo,alisema baadhi ya watu na viongozi wanatumia vibaya rasilimali za umma na kuwapongeza waliosimamia mradi huo kuwa wako karibu na ufalme wa mbinguni na ni wachache wanaoweza kufanya hivyo.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, James Ling’wa,aliwashukuru wananchi kwa walishiriki kujenga mradi huo na kuwezesha majengo kujengwa kwa viwango vya kuridhisha na thamani ya fedha inaonekana.
Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Dr.Sebastian Pima, alisema wanajivunia ilani ya CCM ya kupeleka vituo vya afya kila kata na fedha zinazoletwa na serikali tutazisimamia na kwamba mradi huo utakuwa na faida mbalimbali zikiwemo za rufaa,vifo vya wajawazito na watoto vitapungua,upasuaji wa dharura na wataalamu wataongezwa.