Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Mara Warwick wakisaini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 650 sawa na shilingi trilioni 1.501 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi na mradi wa kuimarisha usalama wa milki za ardhi nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Mara Warwick , wakibadilishana hati za mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 650 sawa na shilingi trilioni 1.501 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi na mradi wa kuimarisha usalama wa miliki za ardhi nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Mhe. Bi. Mara Warwick, wakionesha mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 650 sawa na shilingi trilioni 1.501 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi na mradi wa kuimarisha usalama wa miliki za ardhi nchini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na MIpango)
********************
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA na Benki ya Dunia zimetiliana saini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 650 sawa na shilingi trilioni 1.5 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi (BOOST) na mradi wa kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini.
Mikataba hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Mara Warwick.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, Bw. Tutuba alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia kupitia mgao wa masharti nafuu wa Mzunguko wa IDA 19, ambapo dola za Marekani milioni 500 zitatumika kuboresha elimu ya msingi na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 150 kitatumika kuimarisha usalama wa milki za ardhi hapa nchini.
Bw. Tutuba alisema kuwa miradi iliyo chini ya Mikataba iliyosainiwa inatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) na ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, inayolenga kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu kupitia mikakati mbalimbali.
Alifafanua kuwa katika sekta ya elimu ya msingi, fedha hizo zitatumika kuboresha na kusimamia mazingira shirikishi ya kufundishia na kujifunzia, kuboresha uwezo wa walimu, kukuza na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika shule za awali na msingi.
Mradi wa BOOST unakusudia kuboresha usawa katika upatikanaji wa elimu bora ya awali na msingi kwa upande wa Tanzania Bara ukiwemo ujenzi wa vyumba 12,000 vya madarasa pamoja na vifaa vinavyohitajika vya elimu; usimikaji wa mifumo na usambazaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu 800 kwa pamoja; na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za awali na msingi.
Bw. Tutuba alisema kuwa katika sekta ya ardhi, kazi zitakazofanyika ni kukuza na kuwezesha upangaji, upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi kwa ajili ya uwekezaji na usalama wa makazi ya watu, kuboresha na kuongeza mfumo unganishi wa taarifa za usimamizi wa ardhi na kukuza matumizi ya TEHAMA katika upimaji na uandaaji wa hatimiliki ya ardhi.
“Mradi huu unatarajia kunufaisha nchi kupitia ongezeko la usalama wa umiliki katika wilaya 40 zilizochaguliwa, kwa kutoa hati za Kimila ya Kumiliki Ardhi Vijijini (CCROs), hati za Kumiliki Ardhi Mijini (CROs) na Leseni za Makazi. Aidha, mradi utaongeza ufanisi wa usimamizi wa taarifa za ardhi kupitia uboreshaji wa Mfumo wa Kidijitali wa Taarifa za Ardhi (ILMIS) na utengenezaji wa ramani za msingi (Base Maps)” alifafanua Bw. Tutuba.
Bw. Tutuba alisema kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili kumefanya kiwango fedha kilichowekezwa na Benki ya Dunia hapa nchini kufikia dola za Marekani bilioni 6.15 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Nyanja mbalimbali.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kukushukuru wewe binafsi Bi. Mara Warwick, na kupitia kwako, Benki ya Dunia, kwa mikopo hii muhimu ambayo imekuja katika wakati muafaka” alisema Bw. Tutuba
Aliwaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi na Katibu MKuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka wakasimamie ukamilishaji kwa masharti yote ya awali (conditions of effectiveness) kwa wakati ili kuwezesha kuanza rasmi kwa utekelezaji wa miradi hiyo miwili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Mara Warwick alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha elimu na kwamba fedha zilizotolewa na Benki hiyo kama mkopo nafuu zitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 12,000 wanaosoma masomo ya awali na elimu ya msingi.
Bi. Warwick alisema pia kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha mkopo wa dola za Marekani milioni 150 kwa sababu mpango wa kuimarisha masuala ya ardhi utawanufaisha zaidi ya wananchi milioni 2 hususan waishio vijiji kwa kupatiwa hatimiliki za kimila zaidi ya 500,000 kwenye mikoa 14 yenye wilaya 40.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Elirehema Sedoyeka alisema kuwa dola za Marekani milioni 500 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.15 zitatumika
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi alisema kuwa kiasi cha dola za Marekani milioni 150 zilizoelekezwa katika kuimarisha sekta ya ardhi, zitatumika kusimika mifumo ya kielektroniki katika mikoa 24 kwa kujenga ofisi za ardhi na kufanya ufuatiliaji na tathimini ya mradi.
Alisema kuwa kiasi cha dola milioni 71.9 kitatumika kuongeza usalama wa ardhi, dola milioni 33.1 (menejimenti ya mifumo) dola milioni 24.7 (Maendeleo ya ardhi), dola milioni 12.7 (Menejimenti ya mradi) na dola za Marekani milioni 7.5 zitaelekezwa kwenye masuala ya dharura na kwamba mradi huo utakapokamilika utaongeza mapato ya Serikali kupitia kodi ya pango la ardhi na mapato mengine ya Serikali.