******************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
BAADHI ya wakazi wa Kwamfipa,Kibaha Mkoani Pwani wamesema ujenzi wa barabara ya Ukombozi kuelekea Chuo Cha Uongozi kikubwa Afrika, Mwalimu Julius Nyerere ,ni mkombozi kwao kufungua milango ya kiuchumi .
Aidha wameeleza, wanaishukuru Serikali kwa kujenga Chuo hicho kwani kimesababisha kuleta matokeo chanya ya kimaendeleo kwa kufungua miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami na kuondokana na barabara ya vumbi iliyokuwepo awali.
Mzee Saddy Hengo ,Amina Swale na Zaina Abdul wakizungumzia juu ya uzinduzi wa barabara hiyo yenye takriban kilometa mbili,ambayo inatarajiwa kuzinduliwa February 22 mwaka huu na Katibu mkuu wa CCM Taifa Daniel Chongolo walisema, barabara ya vumbi ilikuwa kero katika usafiri na kutumia muda mrefu kufika eneo husika.
“Kwasasa tunateleza tuu ,ukichukua boda kwenda mahali dakika tano umefika,hakuna kuumia mgongo wala Nini ,kiukweli ujenzi wa chuo cha uongozi umetuletea neema”walisema.
Nae Zaina alisema , wajasiriamali imekuwa vifijo kwao kwani mama lishe, wenye maduka kwasasa milango ya kiuchumi imefunguka kutokana na ongezeko la watu wanaojenga kutokana na kuona miundombinu rafiki.
‘”Sipati picha wanafunzi wakianza, Chuo kikianza ndio kabisa naamini vyakula ,vifaa mbalimbali vitanunulika kwa wingi ,sisi wafanyabiashara Tunashukuru Sana”alisisitiza Zaina.
Vilevile Mzee Hengo alisema , kwenye maendeleo yoyote inatakiwa kuwe na miundombinu rafiki ,hivyo kwasasa Kwamfipa maendeleo yataonekana.
Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge alisema kuwa kwenye uzinduzi wa barabara hiyo makatibu wakuu wa vyama rafiki watashiriki ikiwemo ZANU PF cha Zimbabwe, MPLA cha Angola, SWAPO Namibia FRELIMO Msumbiji na ANC Afrika Kusini.
Baada ya uzinduzi huo wa barabara ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Taifa, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi , katika uzinduzi wa Chuo hicho Februari 23 mwaka huu.