………………………………………………..
Na Sixmund Begashe
Wageni mbalimbali wa ndani na nje wameshauriwa kutembelea Kijiji cha Makumbusho kilichopo Kijitonyama Dar es Salaam kwani ni sehemu sahihi ya kujifunza na kujionea urithi wa Utamaduni wa Makabila mbalimbali ya kitanzania.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Finland nchini Mhe Riitta Swan alipotembelea Makumbusho hiyo akiwa na familia yake.
Balozi Swan amesema, ameona ni vyema aitembeze familia yeke kwenye Makumbusho hiyo ya Kijiji ili waweze kujifunza kuhusu Utamaduni wa mtanzania kupitia Nyumba na vitu vya asili vilivyo hifadhiwa hapo.
Kutokana na jitihada za maboresho ya Makumbusho hiyo ya Kijiji, Balozi Swan ameipongeza Makumbusho ya Taifa chini ya Mkurugenzi Mkuu Dkt Noel Lwoga kwa jitihada hizo ambazo zitaongeza mvuto kwa watalii wa ndani na wa nje kutembelea Makumbusho hiyo.
Mhifadhi Mwandamizi wa Mila wa Makumbusho ya Taifa tawi la Kijiji cha Makumbusho Bw Wilbard Lema, amesema ni faraja kubwa kuona namna Mabalozi wa nchi mbalimbali wakitembelea Kijiji hicho wakiwa kikazi na wakati mwingine kifamilia.
“Tumekuwa tukiwapokea Waheshimiwa Mabalozi wengi hapa Makumbusho wakiwa kikazi na kifamilia, wamekuwa wakitumia siku zao za mapumziko katika kuburudika na kujifunza Utamaduni wetu na wanapo kuwa hapa wanaburudika haswa.” Bw Lema
Bw. Lema aliongeza kuwa kilichofanywa na Balozi Swan ni cha kuigwa na watanzania kutembelea Makumbusho hiyo kifamilia ili kuwarithisha watoto Utamaduni wao.
Hii ni mara ya pili kwa Balozi Swan kutembelea Kijiji cha Makumbusho na Ofisi yake imekuwa ikipeleka wageni mara kadhaa katika Makumbusho hiyo pekee iliyohifadhi urithi wa Nyumba za makabila mbalimbali ya hapa nchini.