Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Festo Kiswaga (Kulia), kushoto ni picha ya mtoto mchanga
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kahama Mhe. Festo Kiswaga amelipongeza Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Msalala Mkoani Shinyanga na wananchi kwa kazi kubwa waliyoifanya kufanikiwa kupatikana kwa mtoto mchanga aliyeibiwa wodini katika Kituo cha Afya Lunguya halmashauri ya Msalala.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 18,2022 Kiswaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kahama amelishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Msalala kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kuhakikisha mtoto huyo anapatikana akiwa na afya njema.
“Vilevile tunawashukuru wananchi wote walio shirikiana na Polisi kuwezesha taarifa muhimu za kupatikana kwa mtoto.Nawaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa Polisi ili tuendelee kuiweka Wilaya yetu katika tulivu na yenye amani”,amesema Kiswaga.
Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo ambalo limevuta hisia za watu wengi amesema mnamo tarehe 1/2/2022 majira ya saa 05:30 kwenye Kituo cha Afya Lunguya kilicho ndani ya Halmashauri ya Msalala mtoto mchanga wa kiume aliyekuwa na siku moja tu tangu kuzaliwa aliibwa akiwa kitandani.
“Mnamo tarehe 30/01/2022 majira ya saa 10:00 Mama wa mtoto huyo aitwaye Bertha Augustino (20) mkazi wa Ntambarare kata ya Segese akitokea Zahanati ya Segese na kupelekwa Kituo cha Afya Lunguya kwa Rufaa, alifanyiwa upasuaji na kujifungua mtoto huyo wa kiume na kubakia wodini kwa uangalizi zaidi wa kitabibu”,amesema Kiswaga.
“Mama huyo akiwa pale wodini kabla na baada ya kujifungua alionekana akipewa huduma zingine na mwanamke mmoja mnene, mweusi, mwenye macho ya makengeza ambaye wauguzi walipotaka kujua mwanamke huyo ana uhusiano gani na mzazi, Mama na Baba wa mtoto walieleza kuwa hawamfahamu.Ndipo ghafla siku hiyo ya tarehe 1/2/2022 majira ya saa 05:30 ilikuja kubainika mtoto huyo ameibwa na mwanamke aliyekuwa akimhudumia mama wa mtoto naye ametoweka”,ameeleza Kiswaga.
Amesema kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi wa tukio hilo mara moja ambako waliweza kufika Geita, Sengerema, Kasulu, Masumbwe na Kahama katika ufuatiliaji wao.
“Mnamo tarehe 16/2/2022 majira ya saa 23:30 usiku huko kijiji cha Kakumbi Kata ya Lubunga Wilaya ya Mbogwe Mkoa wa Geita askari wa Polisi Msalala walifanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aitwaye Rehema Said (47) mkazi wa Lubunga akiwa amelala ndani mwake na mtoto mchanga wa kiume”,amesema.
“Ndugu wanahabari, baada ya kufikishwa Polisi Bugarama Wilaya ya Kipolisi Msalala, wazazi wa mtoto waliweza kumtambua mtoto wao na pia mwanamke huyo alitambuliwa kuwa ndiye aliyekuwa akimsaidia mama wa mtoto na kumuiba pale Kituo cha Afya Lunguya”,ameongeza Kiswaga.
Amesema Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara tu upelelezi wa kesi hii utakapokamilika.