Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Veronica Sayore akiongea na wafaidaka wa mikopo ya asilimia 10 (hawapo pichani) kushoto aliyekaa ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Busega Bw. Dismas Ijagala.
…………………………………………
Vikundi 17 vya wajasiriamali Wilayani Busega vimenufaika na mikopo ya asimilia 10 itokanayo na mapato ya ndani, ambapo kiasi cha TZS milioni 132.54 kimetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kati ya fedha hizo TZS milioni 86.325 kimetokana na mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambayo sawa na asilimia 49.9 na TZS milioni 46.215 kimetokana na marejesho ya mikopo kutoka kwa wafaidika.
Akizungumza wakati alipokutana na vikundi hivyo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Veronica Sayore amesema mikopo hiyo yenye masharti nafuu imetolewa ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya utoaji mikopo kwa wajasiriamali wa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Sayore amevitaka vikundi hivyo kuhakikisha wanazielekeza fedha hizo katika malengo yao waliyojiwekea kwa kila kikundi na sio vinginevyo. “Matumizi ya fedha hizi za mikopo zitumike katika malengo yale mliojiwekea ili kuhakikisha mnarejesha kwa wakati na sio vinginevyo” aliongeza Sayore.
Kwa upande mwingine Sayore amesema kumekuwa na vikundi ambavyo vinashindwa kurudisha fedha za mikopo kwa wakati hivyo hukwamisha shughuli za ukopeshaji kwa wahitaji wengine. “Tunaomba mrudishe mikopo hiyo kwa wakati, ili kusaidia wengine wenye uhitaji wa mikopo hiyo, wale ambao hawarudishi kwa wakati mnakwamisha, sitarajii kuliona hilo kutoka kwenu”, alisema Sayore.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Busega, Dismas Ijagala amewaasa wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa usahihi ili kuepusha sintofahamu wakati wa urejeshwaji wa mikopo hiyo. “Vipo baadhi ya vikundi ambavyo vimekuwa na upotevu wa fedha wanazokopeshwa, hii inasababishwa na kutokuwa na matumizi sahihi ya fedha hizo, alisema Ijagala.
Aidha, Sayore amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya vikundi ambavyo vitaonesha kutorejesha fedha hizo kwa wakati. Halikadhalika, Sayore amesema kupitia mikopo hii ya asilimia 10 ya wajasiriamali itasaidia vikundi hivyo kuongeza mtaji wa shughuli zao za kiuchumi.
Pamoja na hayo, Sayore amevitaka vikundi hivyo kuimarisha umoja ili vikundi hivyo vidumu katika misingi ya kujenga uchumi wa mtu mmojammoja. Kwa upande wa wafaidika wameshukuru kwa mikopo hiyo na kuahidi kuitumia mikopo hiyo kulingana na malengo waliyojiwekea. Halmashauri ya Wilaya ya Busega imetoa kiasi cha fedha hiyo ikiwa ni mpaka kufikia robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo vikundi 12 vya wanawake, vimepata kiasi cha TZS milioni 63.54, vikundi 4 vya vijana TZS milioni 57 na kikundi 1 cha watu wenye ulemavu TZS milioni 12.