Mohameduwais Abdullatif akichapa maji
Romeo Mihaly akiongelea
************************
Dar es Salaam. Klabu tisa zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya kuogelea ya Taliss-IST yaliyopangwa kufanyika Februari 26 na 27 kwenye Bwawa la Kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Masaki.
Meneja wa klabu ya Taliss-IST, Hadija Shebe amezitaja klabu hizo kuwa ni Moshi, Wahoo (Zanzibar), FK Blue Marlins (Dar es Salaam), Dar es Salaam Swimming Club (Dar es Salaam), Bluefins (Dar es Salaam) na Mwanza Swimming Club.
Pia katika orodha hiyo, kuna klabu ya Mis Piranhas (Morogoro), Champions Rise (Dar es Salaam) na wenyeji wa mashindani hao, Taliss-IST.
Hadija alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na waogeleaji wanafanya mazoezi ili kushindania zawadi mbalimbali siku hiyo.
Alisema kuwa waogeleaji zaidi ya 200 wanatarajia kushiriki katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Jubilee Insurance, Azam, Pepsi, Auric Air, Dolphin Tours and Safari limited, Burger 53 na Knight support.
Kwa mujibu wa Hadija, waogeleaji watashindana katika umri tofauti katika staili mbalimbali kwa mujibu wa taratibu. Alisema kuwa kutakuwa na kundi la waogeleaji chini ya miaka 8, 9 na 10, 11 na 12, 13 na 14, na zaidi ya miaka 15.
Alisema kuwa mbali ya staili tano za kuogelea, waogeleaji hao watahsindanai katika relei ambayo kwa mtindo wa Individual Medley (IM) na Freestyle. Kwenye IM, waogeaji watachanganya staili nne ambazo ni butterfly, backstroke, breaststroke, na freestyle.
“Waogeleaji watakaoshinda katika mashindano hayo watazawadiwa medali na vikombe, tunawaomba wadhamini wajitokeze ili kufanikisha mashindano haya ambayo ni maarufu na yenye mvuto mkubwa,” alisema Hadija.