*************************
Adeladius Makwega-DODOMA.
Msomaji wa matini hii nakukumbusha kuwa katika sehemu ya pili nilikueleza namna Wapare walivyofanya utani katika sherehe zao za tohara za wasichana na wavulana na namna walivyokuwa wakiimba katika sherehe hizo.
Leo naendelea na namna maisha ya vijana wa kike na wakiume walivyokuwa wakiishi katika jamii ya Wapare. Mabinti na wavulana ambao walikuwa wamepevuka walikuwa wakiishi katika nyumba maalumu ambayo ilikuwa inafahamika kama BWENI.
Neno hilo BWENI lina asili ya kabila hilo la Wapare likimaanisha nyumba wanayokaa vijana wa rika hilo. Nyumba hiyo ndipo vijana wengi walipata wachumba wa kuoana na kuishi pamoja. Hapo palikuwa ni pahala ambapo vijana hukaa na kutaniana na kubadilishana mawazo.
Katika nyumba hiyo ngoma huandaliwa kwa sherehe kadhaa ambapo zana za muziki kama malimba hupigwa. Katika shughuli hiyo ndipo vijana hujaribu kueleza hisia zao kama kumkubalia mtu au kumkataa. Hapo nyimbo huimbwa katika mitindo ya mashairi yenye ujumbe wa sifa kwa wapenzi, tabia njema na kadhalika.
Wapare pia wana neno lingine linalofahamika kama KINJI, hiki ni kitendo cha kwenda shambani kulinda mazao yaliyokomaa hapo huwa ni wakati wa kulinda mazao hayo ili yavunwe yakiwa salama.
Wakiwa katika malindo hayo hata wakati wa usiku wengine hupanda juu ya mawe huku wakiimba au kuzungumza na wenzao walio katika mashamba mengine kwani sauti husika viizuri sana muda huo. Wakati zoezi hilo la kulinda mazao na wanyama waharibifu likifanyika vijana hao ukoka moto na kuzungumza mambo kadhaa.
Wapare wanao utani katika ndoa lengo nikuongeza ujirani baina yule anayetaniwa na mwenzake.
Ndugu F.A. Mzava ambaye naye ni Mpare katika mojawapo ya kazi zake za utafiti kwa kbaila hili anasema kuwa watani wakubwa wa Wapare ni Wachaga na Wasambaa na jambo hilo linashangaza kuwa Wapare kwa mtu ambaye siyo wa kabila lao humuita MNYAMWEZI lakini Wasambaa na Wachaga kwa Wapare hawaitwi WANYAMWEZI.
Ndugu Mzava anadai kuwa ujirani huo ambao unakuwa sawana na udugu ulivyoimarishwa na ule utani baina yao.
Ndugu Mzava anasema kuwa kuna wakati akiwa kwao Upareni alisimuliwa habari ya ndugu mmoja aliyekuwa na kaka yake na baba yake. Baba yao aliamua siku moja waende kumtembea rafiki yake aliyekuwa jirani na kijiji chao.
Kaka huyo aliyemsimulia Ndugu Mzava waliianza safari hadi huko . Walipofika kwa rafiki wa baba yao walipokelewa. Rafiki wa mzee huyo alimuuliza baba wa hawa vijana:
“Uyoa ni naio ngese nyose.”
Mwenyeji huyo alimaanisha kuwa unakwenda wapi na watu wote hao. Jambo hili liliwaumiza mno vijana hawa, lakini baba yao aliona ni jambo la kawaida tu, akitambua hicho kilichofanyika ni utani.
Kiukweli kabisa jambo hili linaweza kumsababisha yule alikwenda kumtembelea rafiki yake kugeuza na kurudi alipotoka lakini hilo halikufanyika hivyo.
Kuna mfano mwingine kuwa ndugu mmoja alikuwa amesafiri muda mrefu sana na siku hiyo alikuwa akirudi kutoka safari, mara alipita kwa rafiki yake kumsalimia, ndugu huyo alimuuliza eh unatoka wapi? Jamaa aljibiwa kuwa yeye anatoka safarini. Jirani akasema kumbe hautoki nyumbani kwako? Jamaa alijibu ndiyo.
“Tumanyije iti mwana wako afwa.”
Jamaa akamwambia kuwa kwako kuna msiba mwanao amefariki. Kwa kuwa walikuwa watani jamaa huyu hakumtilia maanani alikaa kimya hapo na kunywa zake maji na kuondoka zake
Katika kumalizia kabila hili kumekuwa na maswali ya Imani ya Wapare katika ushirikina.Je Wapare wanaamini katika uchawi? Kulijibu swali hilo F.A. Mzava anasema kuwa;
“Wapare wanaamini katika ushirikina lakini wanaamini kuwa mtani hawezi kumroga mtani mwenzake na ndiyo maana ilikuwa vigumu mno kumsikia Mpare, Msambaa na Mchaga juu tuhuma hizo wakati huo. Ndiyo kusema kila wakati mtani humtakia mema mtani wake.”
Mwanakwetu kwa leo naiweka kalamu yangu chini, nikihitimisha safari ya kabila hili la Wapare na utani ndani yake. Nina hakika kwa kiasi umetambua namna Wapare wanavyofanya utani na watani wao Wasambaa na Wachaga.
Katika matini ijayo nitalitazama kabila la Wangindo, Je Ungidoni kuna nini? Subiri matini ijayo.
Nakutakia siku njema.