Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),
Sheikh Abdullah bin Zayed tarehe 13 februari 2022 ametembelea Banda la Tanzania
kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini
humo, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Banda la
Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Baada ya
kuwasili kwenye banda hilo na kutembezwa, Mhe. Zayed aliipongeza Tanzania kwa kuandaa
Banda lenye mvuto na linaloonyesha vivutio vya utalii pamoja na fursa zilizopo
katika sekta mbalimbali kama za utalii, nishati, uchukuzi na madini.
Kwa upande
wake, Mhe. Balozi alimshukuru Mgeni wake kwa kuchagua kutembelea banda la Tanzania
ikiwa ni moja ya nchi 192 zinazoshiriki maonesho hayo. Aidha, aliishukuru
Serikali ya UAE kwa kuandaa vizuri Maonesho makubwa ya Expo 2020 Dubai, licha
ya uwepo wa changamoto ya kuenea kwa ugonjwa wa COVID -19.
Ushiriki
wa Tanzania unatarajiwa kuwa na matokeo chanya na kuongeza idadi ya Watalii
watakaoitembelea Tanzania, wawekezaji, mitaji pamoja na masoko ya bidhaa
zinazozalishwa nchini. Katika Maonesho haya, Tanzania ni miongoni mwa nchi 50
ambapo kwa mara ya kwanza zinashiriki kwenye mabanda pekee
yaliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya UAE.
Katika hatua
nyingine, Ubalozi wa Tanzania, UAE utasherehekea Siku ya Kitaifa (National Day)
tarehe 27 Februari 2022. Sherehe hizo zitapambwa na shughuli mbalimbali
zikiwemo Kongamano kubwa la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika kwenye Ukumbi
wa Ballon, Hoteli ya Jumeirah Beach tarehe 27 Februari 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed akiangalia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini inayooneshwa kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai. |