…………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini kwa kusaidiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha , vyuo vya ualimu nchini vinaweza kujiendesha ili kuongeza tija ufanisi katika uendeshaji wake.
Katika kufikia azma hiyo, wajumbe wa bodi hizo waliaswa kuwa wabunifu na kutumia muda wao kufikiri namna mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, vyuo hivyo vinaweza kujiendesha ikiwemo kutoa ushauri wa uanzishaji na uendelezaji wa miradi yenye tija vyuoni.
Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi za vyuo vya ualimu nchini yaliyoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Nchini (ADEM) katika kampasi ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Aliwasisitiza kufuata sheria, kanuni, sera za elimu pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
Profesa Mdoe alisema, serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika vyuo vya ualimu nchini kwa lengo la kuwapata walimu wenye vigezo stahiki kwa mahitaji ya sasa na baadaye.
“Dhima ya vyuo vya ualimu nchini ni kuandaa walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji katika shule za awali, msingi na sekondari. Kutokana na dhima hiyo, serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika vyuo vyote vya ualimu nchini” alisema Profesa Mdoe
“Bodi za vyuo vya ualimu ni kiungo muhimu kati ya chuo na wizara lakini pia ni kiungo kati ya chuo na jamii, , kwa maana hiyo bodi zina jukumu la kuwashirikisha wadau katika kuchangia maendeleo ya chuo kupitia uchangiaji wa rasilimali na hata utaalamu” alisisitiza Profesa Mdoe
Akizungumzia mchango wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Nchini (ADEM), Naibu Katibu Mkuu huyo alifurahishwa na utendaji kazi wake, hususan wanapotimiza majukumu ya kusimamia na uendeshaji wa mafunzo kazini kwa walimu na viongozi wa elimu nchini na kuwa mhimili muhimu katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Nawapongeza Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Nchini (ADEM) kwa kuandaa na kuendesha mafunzo kwa Wajumbe wa Bodi za Ushauri za Vyuo vya Ualimu nchini, Aidha, Wizara ya Elimu inathamini kazi yenu ya uendeshaji wa mafunzo kazini kwa walimu na viongozi wa elimu” alibainisha Profesa Mdoe
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Nchini (ADEM), Dkt. Siston Masanja amesema, mafunzo yote wanayoyatoa kupitia wakala huo yanalenga kuwapa washiriki maarifa, ujuzi na uwezo wa kubadilika mara baada ya kupokea mafunzo husika hivyo amewataka washiriki kwenda kuyatumia mafunzo haya kwa lengo la kuleta tija kwenye vyuo vya ualimu.
“Mafunzo yoyote yanalenga maarifa, ujuzi na uwezo wa kubadilika mara baada ya kupokea mafunzo, “
“Kubadilika mara baada ya kupata mafunzo, ndio kunakuwa na changamoto kwa watu wengi, kwani wanaweza kuwa wamepata maarifa na ujuzi, lakini maamuzi ya kutumia maarifa na ujuzi huo ndio panakuwa na changamoto, hivyo basi sisi kama ADEM tutafutailia eneo hilo na kufanya tathimini pindi washiriki watakaporudi kwenye majukumu yao”
Mmoja wa washiriki wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ualimu Morogoro, Dkt. Noah Mtana alisema wamepata mwanga na uelewa,kuyafahamu majukumu yao vyema sanjari na kuwapatia nyenzo muhimu za utekelezaji wa majukumu yao .
Mafunzo ya siku saba yenye lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi za vyuo vya ualimu nchini yameendeshwa na kusimamiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Nchini (ADEM) ambapo jumla ya washiriki 406 wameshiriki na kuhitimu mafunzo hayo kutoka vyuo vya ualimu vya serikali nchini .