Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Julieth Kidemi akipokea cheti cha namba ya utambulisho wa mlipakodi kutoka kwa mfanyabiashara wa Shirati wilayani Tarime mkoani Mara kwa ajili ya kuangalia taarifa zake wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani humo.
Afisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Deusdedith Mwanzalima akitoa elimu kuhusu athari za magendo kwa wakazi wanaoishi eneo la Mtimrabu ambalo ni mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Mara.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Lameck Ndinda akitoa elimu kuhusu athari za magendo kwa wakazi wanaoishi eneo la Mtimrabu ambalo ni mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Mara.Wakazi wanaoishi eneo la Mtimrabu ambalo ni mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya wakipata elimu kuhusu athari za magendo kutoka kwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Mara.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Edwin Iwato akitoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wa Shirati wilayani Tarime mkoani Mara wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani humo.
Afisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Deusdedith Mwanzalima akitoa elimu juu ya umuhimu wa kudai risiti kwa mfanyabiashara mdogo wa Shirati wilayani Tarime mkoani Mara wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani humo. (PICHA ZOTE NA TRA).
*******************
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaelimisha wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla kuhusu athari za magendo ya kwamba licha ya kuikosesha serikali mapato, zinaweza pia kuhatarisha afya za walaji.
Akizungumza wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango inayoendelea mkoani Mara, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa TRA Bw. Stephen Kauzeni amesema kuwa, ni muhimu wafanyabiashara wakapitisha bidhaa katika njia rasmi ili kuhakikisha kwamba kila bidhaa inayoingia nchini inakaguliwa ubora wake kwa lengo la kulinda afya za walaji.
“Athari nyingine ya magendo ni nchi kukosa takwimu sahihi za bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, kukosekana kwa ushindani sawia wa wafanyabiashara kutokana na wengine kuuza bei za juu kwasababu wamelipia ushuru na wengine kuuza bei za chini kutokana na kupitisha bidhaa kwenye njia zisizo rasmi,” alisema Bw. Kauzeni.
Kwa upande wake Afisa Msimamizi wa Kodi wa TRA Bi. Julieth Kidemi ameeleza kuwa, serikali inategemea kodi ili iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi kwa kupitisha bidhaa kwenye njia zisizo rasmi wanaichelewesha nchi kupiga hatua.
“Ndugu zangu kupitia kodi tunazolipa nchi yetu inajenga miundombinu ya reli, barabara, inalipa mishahara ya watumishi, inajenga shule na mambo mengine kama hayo hivyo nawasihi tuache magendo na tulipe kodi kwa hiari”, alisema Bi. Julieth.
Nao wakazi wanaoishi eneo la Mtimrabu ambalo ni mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania kujenga ofisi ya TRA katika eneo hilo ili waweze kupata huduma za kiforodha na kuondoa usumbufu wa kufuata huduma hizo katika mpaka wa Sirari.
“Leo tumefurahi sana kutembelewa na maofisa wa TRA ambao wametupatia elimu juu athari za magendo lakini sisi wakazi wa hapa Mtimrabu tunaiomba serikali itujengee ofisi ya TRA maana tunahangaika sana kufuata huduma za forodha Sirari”, alisema Bw. Paulo Moti ambaye ni mkazi wa eneo hilo.
Naye, Mwita Juma ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo la Mtimrabu amesema kwamba, kitendo cha kutokuwepo kwa ofisi ya TRA katika eneo hilo kinachochea watu wengi kufanya magendo suala linaloisababisha serikali kukosa mapato.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani Mara ilianza tarehe 7 na itamalizika tarehe 21 Februari, 2022 ambapo baada ya kumaliza kampeni hiyo katika Wilaya ya Tarime, maofisa wa TRA wataelekea katika Wilaya ya Bunda.