Adeladius Makwega-DODOMA
Miaka ya 1980 mwishoni na 1990 mwanzoni nilikuwa na marafiki zangu wawili mmoja anaitwa Bakari Bakari Membe na mwingine anafahamika kama Juma Seifu. Hawa jamaa wote walikuwa wanafunzi wa shule za msingi na baadaye sekondari. Membe alikuwa akisoma Kibasila Sekondari naye Seifu akisoma Azania Sekondari, zote za Dar es Salaam.
Ndugu hawa nilikuwa nawafahamu tangu wakiwa vijana wadogo na hata wazazi na walezi wao niliwafahamu kwa majina na tabia.
Membe alikaa na wazazi wake ambao walikuwa wafanyabiashara wa soko la Mbagala Kizuiani na Seifu alikuwa anaishi na kaka zake nao pia walikuwa wafanyabishara Sokoni Kizuiani Mbagala na Sokoni Tandika.
Wazazi na walezi wa ndugu zangu hawa walikuwa wakijipatia kipato chao cha kila siku kwa biashara za sokoni. Nakumbuka rafiki zangu hawa walisoma vizuri huku wakipatiwa mahitaji yote muhimu ya mwanafunzi kuliko hata ya wazazi wa wanafunzi waliokuwa watumishi wa umma.
Nakumbuka wakati wa likizo siye tukibaki nyumbani kucheza mpira wezangu hawa walikuwa wakienda kushinda sokoni kuwasaidia wazazi na walezi wao katika biashara hizo sokoini.
Hata mimi nilipokuwa nikichoka kucheza mpira hufunga safari hadi Sokoni Kizuiani kuwafuata ndugu zangu hawa kuzungumza nao. Hiyo haimaanishi kuwa kwetu hakukuwa na biashara, zilikuwapo lakini hazikuwa za mtaji mkubwa kama za sokoni kwa hawa rafiki zangu.
Ndugu zangu hawa hadi sasa ni wafanyabiashara kwenye masoko haya lakini sasa wana mitaji yao wenyewe na ni mitaji mikubwa. Wezangu somo la ujasiliamali liliwaingia vizuri.
Wiki iliyopita niliposikia kuwa kuna Soko la Mbagala limeungua moto, mawazo yangu yote yaliwakumbuka ndugu hawa. Nilikumbuka tangu tulivyokuwa tunasoma nao na namna walivyokuwa wakijifunza biashara wakati huo tukiwa wadogo.
Nikasema kuwa ndugu zangu hawa wana familia zenye wanawake tena zaidi mmoja kulingana na imani yao ya dini alafu pia wana watoto kadhaa na Bakari Membe mwenzetu ameshajaliwa kujukuu, sasa nikajiuliza kama soko lao limeungua, je itakuwaje?
Kabla ya kuwatafuwa ndugu hawa nijue kilichotokea nilimpigia simu Diwani wa Mbagala mheshimiwa Michael Makwega kumuuliza kulikoni? Yeye akanijibu kuwa soko lililoungua ni la huko Mbagala Zakhem.
Nilibaini kuwa Bakari na Juma soko lao halijaungua kwa hiyo kuwapigia simu nikaona hilo halina maana. Nikiwa nyumbani kwangu nilitafakari matukio haya ya moto kuunguza masoko namna yanavyoleta hasara mto kwa wafanyabiashara
Nikajiuliza je matukio haya ya moto ya kuunguza masoko yanazuiwaje? Nilitafakari na kujipatia majibu kuwa sasa tufanye haya:
Kwanza niliona kuna umuhimu mkubwa wa wafanyabiashara wenyewe kutambuana katika soko lao na kazi hiyo ifanywe na viongozi wa soko husika.
Wakishatambuana watajua idadi ya wafanyabishara wote mathalani Soko Z lina wafanyabiashara 490, kisha wanapaswa kutambua mitaji ni kiasi gani ya kila mfanyabiashara katika mkundi matatu Z 1 mtaji mdogo, Z 2 mtaji wa kati na Z 3 mtaji mkubwa.
Katika wafanyabiashara 490 watakuwa katika mgawanyiko huu Z 1-210, Z 2 -150 na
Z 3 -130. Hilo likishafanyika, pia watambue idadi ya wanaume na wanawake. Kwa mfano hapo wanawake watakuwa 230 na wanaume 260.
Ukishamaliza hivyo watambue wazee, wagonjwa, wajawazito na wenye watoto wadogo. Hapo unaweza kupata watu 90 kwa hiyo utabaki na watu 400, hawa watakuwa ni nguvu kazi ya soko Z.
Kwa watu hawa 400 wagawe katika magenge ya watu 10 kwa 10 ndiyo kusema kutakuwa na magenge 40. Kwa kuwa mwezi una siku 30-31 magenge 30 yatatumika, tumia genge la watu kumi kila siku ndiyo kusema magenge 10 yatabaki kutakuwepo na magenge dharura na magenge mengine yatakuwepo katika mzunguko huo wa kulinda soko lao kwa zamu.
Mkishamaliza mpango huo wafanyabishara wote waitishwe kikao cha pamoja waelezwe mpango huo wa kulinda soko lao wao wenyewe. Huku wale walinzi wa awali wa soko waliopo wakiendelea na kazi kwa kuwa wao wana mafunzo ya ulinzi na matumizi ya silaha.
Tambueni eneo liliopo soko lenu je lina milango mingapi ambayo inapitika na majirani ni kina nani katika soko hilo. Shirikisheni walinzi hao wa awali na kazi ya ulinzi ifanyike. Kwa magenge 40 mtu mmoja atalinda mara moja kwa kila baada ya mwezi mmoja na siku 10.
Wakati yanapangwa magenge ya watu kumi kwa kumi hakikisha Z 1, Z 2 na Z 3 wanachanganywa ipasavyo kila kundi wanatoka watu watatu waje kulinda mali zao ili kuepusha watu wenye biashara za aina moja kulinda wao pekee
Majina ya wanaolinda kila siku apatiwa Mlinzi wa Amani wa mtaa na Kituo cha Polisi jirani. Hiyo ngome ya Z 1, Z 2 na Z 3 hakuna mwenye kuwezo kujaribu kuisogelea. Je teja au mtu yoyote mwenye hila na husuda na masoko hawezi kupenya mwanakwetu. Hapo lazima mali za wafanyabiashara zitalindwa ipasavyo.
Hapo hata mambo ya kumtafuta mchawi pale tatizo likitokea hayatokuwapo tena maana hata kama linatokea tukio hilo wenye mali na mashahidi watakuwepo kuwaambia wafanyabiashara wenzao kilichotokea.
Natambua wafanyabiashara hawa wa masokoni wanatenganishwa na mitaji yao lakini kiukweli wanaunganishwa na madhara ya matukio haya ya moto yanapotokea. Kwa hiyo kuzuia masoko kuungua moto wafanyabiashara wanaweza kuanzisha ulinzi shirikishi wa masoko yao wenyewe.
Mwanakwetu nakwambia soko haliwezi kuungua tena hiyo itabaki katika simulizi tu.
Nakutakia siku njema.