Watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza wakiuliza maswali wakati wa mafunzo ya kutoa uelewa wa magonjwa hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliopo jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo ya siku moja yaliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) ambapo washiriki walikuwa 30 kutoka mikoa mbalimbali.
Watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza wakisikiza mada ya jinsi ya kutoa elimu kwa wagonjwa wenzao ilitokuwa inatolewa na Elizabeth Licoco wakati wa mafunzo ya kutoa uelewa wa magonjwa hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliopo jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo ya siku moja yaliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) ambapo washiriki walikuwa 30 kutoka mikoa mbalimbali.
Msaikolojia tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Idara ya Afya na magonjwa ya akili Isaac Lema akitoa mada ya afya ya akili kwenye mafunzo ya kutoa uelewa wa magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wanaoishi na magonjwa hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof Andrew Swai akitoa mada ya mtindo bora wa maisha kwenye mafunzo ya kutoa uelewa wa magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wanaoishi na magonjwa hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliopo jijini Dar es Salaam.
Picha na Henrick Chiwangu
………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
14/02/2022 Serikali imeombwa kutoa elimu kinga ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo umuhimu wa kudumisha afya ya akili kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kufanya hivyo kutawasaidia kutambua umuhimu wa afya na kufanya uchunguzi wa magonjwa hayo na kuziendea huduma mapema zaidi.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Msaikolojia tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Idara ya Afya na magonjwa ya akili Isaac Lema wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya kutoa uelewa wa magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wanaoishi na magonjwa hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) uliopo jijini Dar es Salaam.
Lema alisema matatizo ya afya ya akili yanatokana na mtu kuwa na kiwango kikubwa cha msongo wa mawazo, na watu wengi wanaokabiliwa na matatizo haya wanakaa kimya na kutowashirikisha watu wa karibu yao au wataalamu hivyo kuwafanya kupelekea mabadiliko ya kitabia, kihisia, kifikra na mwitikio wa mwili.
“Wapo wanaokata tamaa ,kuwa na majonzi, kushindwa kudhibiti hisia kama vile hasira. Kwa upande wa tabia ni matumizi ya vilevi yaliyopindukia, kukosa usingizi, kushindwa kujiamini na kutawaliwa na mawazo hasi”,.
“Njia ya kuondokana na matatizo ya afya ya akili ni pamoja na kudhibiti msongo kwa kufanya mazoezi kila siku, kujitofautisha yeye na tatizo lake alilonalo, kumtofatisha mtu na tatizo lililopo, kutafuta suluhu ya migogoro uliyonayo au kutokuwa na migogoro. Kumbuka kila mtu hukabiliwa na msongo hivyo tunapoutawala tunazuia msongo kujitokeza mara kwa mara au kuwa endelevu”, alisema Lema.
Msaikolojia tiba huyo alisema iwapo mbinu hizo hazitatoa unaafuu uliotarajiwa na iwapo msongo bado utakuwepo kwa kiwango cha juu muhusika asisite kuwaona wataalamu wa afya ya akili.
Lema alisema “Unapobakia kwenye matatizo hayo unaongeza hali ya uhatarishi wa kupata dalili za ugonjwa wa akili kumbuka uwezo wa kufurahia maisha hutokana na afya bora ya akili furaha ya maisha hutokana na afya bora ya akili”,.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof Andrew Swai alisema mwaka 2010 aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili alitumia dawa aina mbili ambazo ni za vidonge na sindano mara mbili kwa siku na akaamua kupunguza uzito hadi kufikia kilo 60 kwani alikuwa na uzito mkubwa zaidi ya kilo 70.
Prof. Swai alisema tangu mwaka 2011 alipopungua uzito hajatumia tena dawa za kisukari kwani ugonjwa wa kisukari aina ya pili wengi wanaupata wakiwa watu wazima. Ukiwa na ugonjwa aina hiyo unaweza kupona kwasababu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanatokana na mtindo mbaya wa maisha wa kutokufanya mazoezi na kula vyakula bila kufuata mpangilio lakini unaweza kuyaepuka kwa kufanya mazoezi na kula vyakula sahihi kwa wakati sahihi.
“Tumeamua kuwafundisha watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni moyo, sukari, pumu, saratani, magonjwa ya akili na selimundu ili wawe na uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa haya, kutokana na uchache wa wataalamu waliopo njia mojawapo ya kutatua tatizo hili ni kuwatumia wagonjwa wenyewe kutoa elimu kwa wenzao”,.
“Kuna wagonjwa ambao wameugua muda mrefu na wanauelewa wa kutosha kuhusu magonjwa haya hivyo basi wagonjwa hawa wanaweza kuwafundisha wagonjwa wengine kupitia kitabu cha mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambuliza ambacho kimeandaliwa na wataalamu wa magonjwa hayo”, alisema Prof.Swai.
Alisema mpango mwingine waliokuwa nao ni kuwafundisha madaktari na wauguzi kutoka vituo vya afya 500, kila kituo watawafundisha wauguzi wawili na madaktari wawili ambao watasaidia kuwafundisha wagonjwa wakati wanasubiri kupata huduma”, alisema Prof. Swai.
Alizitaja changamoto wanayokabiliana nazo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha ili waweze kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari kwa kuandaa vipindi vya redio na televisheni ambavyo siyo bure vinahitaji kulipiwa, aliwaomba wadau wa maendeleo waweze kushirikiana na TANCDA ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Nao wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza walisema katika upatikanaji wa matibabu watakutana na changamoto mbalimbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokupewa elimu ya kutosha kuhusu magonjwa hayo na upatikanaji wa dawa hasa kwa wagonjwa wa kisukari.
Jenipher Kyala mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam alisema mwaka 2019 alipata tatizo la afya ya akili ambalo lilitokana na msongo wa mawazo ya kazi aliokuwa nao hakumwambia mtu yeyote kutokana na tatizo alilokuwa nalo kwani alijuwa ataweza kulitatua yeye mwenyewe.
“Ninakumbuka kuna siku niliamka nikasikia ndani yangu kuna msukumo wa kufanya kitu fulani, nilifanya vurugu nikiwa saluni ndugu zangu walinikamata na kunipeleka Hospitali ya Taifa Muhimbiili (MNH) nikatibiwa na hivi sasa nimepona kama unavyoniona kwani ugonjwa huu unatibika kama magonjwa mengine na watu wanapona na wanaendelea na maisha kama kawaida”,
“Katika jamii yetu watu wanamsongo wa mawazo lakini hawaongei ninawasihi muongee matatizo mliyonayo msijifungie na kufikiria kuwa mtaweza kuyatatua nyinyi wenyewe. Changamoto kubwa niliyokutana nayo wakati ninaumwa ni kutokubalika katika jamii kwani nilifukuzwa kazi kwa ajili ya ugonjwa. pia vigumu kupata kibali cha kufanya jambo fulani”, alisema Jenipher.
Juma Bahati mkazi wa jijini Dar es Salaam alisema akiwa na umri wa miaka 14 alianza kutokwa na jasho jingi, kunywa maji mengi na kupata haja ndogo mara kwa mara hasa wakati wa usiku baada ya kufanyiwa vipimo mwaka 2009 aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza hivi sasa anamiaka 12 anaishi na ugonjwa huo.
Bahati alisema watu wengi katika jamii hawaamini kuwa mtoto mdogo anaweza kupata ugonjwa wa kisukari na akipata ugonjwa huo wanaamini wanaamini kuwa karogwa lakini ukweli ni kuwa hata watoto wadogo wanapata ugonjwa huo kama alivyopata yeye.
“Wazazi wakiwa wanaenda kupima afya zao wawapime na watoto ambao wameambatana nao kwani hata wao wanaweza kuwa na ugonjwa huo pia wakijua wanasukari itawasaidia kupata tiba mapema:, alisema Bahati.
Naye Erick Mtei mkazi wa Kilimanjaro ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya pua alisema akiwa na umri wa miaka 19 alipata tatizo la nyama za pua baada ya kwenda katika Hospitali ya Kanda ya KCMC alifanyiwa upasuaji lakini tatizo likaendelea.
“Ninawashauri wananchi wenzangu wakiona kuna kitu ambacho hakiko sawa katika miili yao waende Hospitali kwa wakati kupima, mimi nilizembea kwenda kutibiwa mapema baada ya kuona shida imezidi mwaka 2015 ndiyo nikaenda kutibiwa”,.
“Sasa hivi ninapata matibabu yangu katika Taasisi ya Saratani ya Oceanroad ninaishukuru Serikali kwani dawa ziko za kutosha na hakuna unyanyapaa wowote ninaoupata kutoka kwa watoa huduma za afya pamoja na jamii inayonizunguka”, alisema Mtei.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) ambapo washiriki ambao ni watu wanaoishi na magonjwa hayo walikuwa walikuwa 30 kutoka mikoa ya Arusha, Kigoma, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro na Dar es Salaam.