………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Wanawake wilayani Kibaha, Mkoani Pwani,wameaswa kujithamini na kuacha kudharau biashara zao wanazozianzisha ili ziweze kukua na kujiongezea kipato.
Aidha amewataka watumie fursa ya mikopo hasa ya Halmashauri kukuza biashara zao na kuthubutu kuanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ,ambae pia ni Diwani wa Sofu Mussa Ndomba alitoa Rai hiyo katika ufunguzi wa kongamano na mafunzo ya ujasiliamali kata ya Mkuza,chini ya mkufunzi Elina Mgonja ambayo yameandaliwa na kanisa la Ufufuo na Uzima, Kibaha, Kwamatias,Jimbo la Pwani
Alieleza ,Vikundi vya ujasiliamali vijengewe uwezo na kuweza kujiendesha ili kujiendeleza kiuchumi.
Ndomba alifafanua ni wakati wa akinamama na vikundi vya ujasiliamali kutumia fursa zilizopo kwa maslahi yao ya kimaendeleo.
“Wanawake hakuna kulala,mjithamini ,muache uoga kuanzisha biashara kubwa ama viwanda mkithubutu mnaweza , Tumieni mikopo hii kujiendeleza na kuachana na utegemezi”
“Serikali ya awamu ya sita imeelekeza Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili yenu ,hivyo changamkieni fursa hii na kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwani Lengo lake ni jema kupigania wajasiriamali”alibainisha Ndomba.
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mji ,Elina Mgonja alisema mafunzo hayo ya ujasiliamali ni ya siku tano yanalenga kuongeza ujuzi kwenye ujasiliamali na usindikaji wa kisasa kwa viwango.
Alisema Ni wakati wa wanawake kujikomboa kwa kujiletea maendeleo.
Mgonja alisema, wanajifunza kwa nadharia na vitendo,na kwahakika mafunzo yataleta tija na hatimae kupata soko la uhakika.
Askofu Maximillian Machumu Kadutu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Kibaha, Kwamatias,Jimbo la Pwani alisema ,mafunzo hayo yatakuwa endelevu na wao wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
“Rais ni mama yetu ,mlezi wa Familia ,na kwasababu hii tutaendelea kuwainua wanawake kwa namna yoyote ile ,Pia nimekubali kuwezesha mashine ya usindikaji ,tunaomba tu Serikali utusaidie eneo na miundombinu Kama umeme”alieleza Kadutu.