Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Kaliua Mkoani Tabora Mhandisi Robert Kisandu akiwasilisha taarifa ya Mikakati ya kuzifanyia Matengenezo barabara zote katika mwaka wa fedha 2022/2023 katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo
………………………………………………………….
Na Lucas Raphael,Tabora
MADIWANI wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamepongeza mikakati mizuri ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilayani humo kuzifanyia matengenezo barabara zote za Mijini na Vijijini kwani zitachochea uchumi wa wananchi, halmashauri na taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa katika kikao maalumu cha baraza kilichofanyika juzi katika ukumbi wa halmashauri walipokuwa wakichangia hoja baada ya TARURA kuwasilishwa taarifa ya utekelezaji miradi ya barabara kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Diwani wa kata ya Kaliua Nestory Hoka, alisema kuwa taarifa ya TARURA imewapata matumaini mapya wananchi hasa ikizingatiwa kuwa barabara zao zimekuwa hazipitiki kwa muda mrefu na kuleta adha kubwa.
Alisema kutengenezwa kwa barabara hizo kutainua uchumi wa wananchi na kumaliza kilio chao cha muda mrefu, alipongeza serikali kwa kupeleka fedha za kutosha katika majimbo yote kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
Naye diwani wa kata ya Kamsekwa Selina Manamba alishauri vijiji ambavyo havina barabara za uhakika zifunguliwe na kusajiliwa ili kuwarahisishia usafiri na usafirishaji mazao yao.
‘Naishukuru serikali kwa kusikia kilio chetu, naomba bajeti ijayo vijiji na maeneo mengine ambayo hayana barabara za uhakika yapewe kipaumbele ili kuinua uchumi wetu’, alisema.
Mwenyekiti Mstaafu wa halmashauri hiyo Haruna Kasele ambaye ni diwani wa kata ya Kazaroho licha ya kupongeza bajeti hiyo aliwataka viongozi kuwapa ushirikiano TARURA na kuhakikisha miundombinu ya barabara inalindwa.
Aidha aliomba elimu kutolewa kwa wananchi hasa jamii ya wafugaji ili waache kupitisha mifugo yao kwenye miundombinu itakayotengenezwa huku akiomba TARURA kutengeneza vivuko na barabara mbadala za kupitishia mifugo.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Jafael Lufungija aliwahakikishia madiwani ambao barabara zao hazipo kwenye bajeti ya mwaka huu licha ya kuzitolea taarifa mapema kuwa zitaingizwa kwenye mpango wa bajeti ijayo, aliwataka kuwa na imani kubwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.