Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Dar Es salaam, Bw Mawazo Ramadhani Jamvi, akiongea kwenye program ya Kijiji Soko, Kijiji cha Makumbusho
Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Dar Es salaam, Bw Mawazo Ramadhani Jamvi akipatiwa maelezo kutoka kwa mmoja wa wasanii kuhusu kinyago kwenye program ya Kijiji Soko, Kijiji cha Makumbusho
Mkazi wa Dar es Salaam akichagua nyama choma ya Swala, kwenye program ya Kijiji Soko.
Baadhi ya wageni mbalimbali walioudhuria Kijiji Soko wakijipatia vinywaji na Nyama Pori.
……………………………………………….
Na Sixmund J. Begashe
Wasanii na wananchi mbambali wamehitajika kutumia fursa iliyotolewa na Serikali kupitia Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam inayoendesha program ya Kijiji Soko ili waweze kunufaika na mazao ya sanaa za kitanzania kwa wasanii kuuza kazi zao na wananchi wasio wasanii kujifunza, kuburudika na kununua kazi za wasanii hao kwa kuwa program hiyo ni ya kwao.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Bw Mawazo Ramadhani Jamvi kwenye gulio la Kazi za Sanaa na wajasiliamali wa tiba lishe linaloendelea kwenye viwanja vya Makumbusho hiyo iliyopo Kijitonyama Dar es Salaam.
Bw Jamvi licha ya kuelezea malengo ya kuanzishwa kwa program hiyo ya Kijiji Soko kuwa ni kuwaleta pamoja wasanii nguli na chipukizi ili wakutane na watumiaji wa kazi za sanaa.
Kaimu Mkueugenzi wa Kijiji cha Makumbusho ameushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii nchini chini ya Waziri Mhe. Dkt Damas Ndumbaro (MB) kwa kutoa kibali cha kuwepo na nyama za wanya pori kitu kinacho saidia kuvuta watu wengi kwenye gulio hilo.
“Gulio hili la kazi za Sanaa limechagizwa na nyama pori, watu ni wengi wanaokuja kujipatia bidhaa, kula nyama za wanyama wa porini, kama Nyati, Swala na nyinginezo, sisi kama waandaaji hakika tumefarijika sana na ni imani yetu kuwa Kijiji Soko kinachofuata watu watakuwa wengi zaidi”. Bw, Jamvi
Akizungumzia mafanikio anayoyapata kwenye Kijiji Soko, Mjasiria Mali wa Tiba Lishe, Bi Happy Vatinga amesema licha ya kupata nafasi ya kuuza bidhaa zake lakini amepata nafasi ya kukutana na wajasiliamali wenzake wenye uzoefu zaidi na kubadilishana uzoefu wa kibiashara pamoja na kupanua wigo wa wateja wa kimataifa.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria Gulio hili, kweli limenipa nafasi ya kukutana na wageni wengi wa ndani na nje ya nchi, kubadilishana mawasiliano, licha ya kuuza hapa naamini nitafanya biasha zaidi baada ya hapa, naishukuru sana Serikali kwa ubunifu huu uliotupa fursa sisi wafanya biasha wadogowadogo”. Anasema Bi Vatinga
Naye mkazi wa Dar es Salaam ajulikanaye kama Babu Iddi, licha ya kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa kuendesha Kijiji Soko, ametoa wito kwa watu mbalimbali kujitokeza na kuwaunga mkono wasanii wa kazi za ufundi kwa kufika kwenye gulio hilo ili waweze kuburudika kwa kazi za Sanaa na vyakula vya asili ikiwemo nyama choma ya wanyama pori.
“Doh! hakika siku yangu imekuwa njema sana, nasikitika kwa kuwa sikuja na familia yangu, nimeumia kwa kweli, sikudhani kama ningeweza kuburudika na kuona kazi nzuri hivi za wasanii wetu, mimi na marafiki zangu tumekula sana nyama ya swala ambayo ni adimu sana kuipata, nashauri wazidishe matangazo ili kila mmoja ajue na aje kufaidika na program hii”. Alimalia Bw Iddi
Gulio hilo la kazi za Sanaa linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 15 Februari 2022 sanjari na uzinduzi wa mradi wa kuboresha nyumba za asili Makumbusho hiyo ya Kijiji, mradi ambao ni kati ya Miradi 15 ya Makumbusho ya Taifa ambayo ni sehemu ya miradi ya ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19 utakaozinduliwa na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael