Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel(wenye kipaza sauti) akitoa maelezo leo kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati wa ziara yao ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama akitoa maoni ya wenzake leo mjini Dodoma kwa niaba ya wajumbe wenzake wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama ya Tanzania .
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel(wenye vazi la bluu) akiwa katika picha ya pamoja leo na Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati wa ziara yao ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Mwingine katika picha ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene( wa saba kutoka kushoto kwa waliosimama)
Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakiwa katika picha ya pamoja leo mara baada ya ziara yao kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania. Mwingine katika picha ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene( wa saba kutoka kushoto kwa waliosimama)
Picha na Mahakama ya Tanzania
**********************
Na Tiganya Vincent- Mahakama
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeridhika maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania unaoendelea mjini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya wajumbe wenzake wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama hiyo.
Amesema wakiwa wamefurahishwa na kazi kubwa ambayo imekwishafanyika katika kusimamia na kuutekeleza mradi huo kwa kiwango cha hali ya juu.
Dkt.Mhagama ameongeza kupitia mradi huo ambao unatokana na fedha zilizotolewa na Serikali inaonyesha dhamira ya dhati ya Mhe.Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyokusudia miguu ya mihimili yote Serikali iwe pamoja mjini Dodoma.
Aidha Kamati hiyo imeridhika na hatua zinazochukuliwa za kuzingatia usalama wa wafanyakazi wanaotekeleza kazi kwenye mradi na utoaji fursa kubwa za ajira nyingi kwa watumishi ambao ni raia wa Kitanzania.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria Mhe .George Simbachawene amesema maendeleo ya ujenzi huo ni kielelezo na alama kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha itatimiza ndoto za siku nyingi za kutaka mihimili yote ya Serikali iwe katika makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma Dodoma.
Amesema mihimili mingine kama vile Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , na Serikali tayari imeshahamia Dodoma na kukamilika kwa Jengo la Mahakama mihimili yote itakuwa pamoja Dodoma.
“Pongezi tunazitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuwezesha muhimi wa Mahakama kifedha ili nao uweze kuhamia Dodoma …hatua hiyo itaifanya Dodoma kuwa Capital City ya Tanzania kwa vitendo” amesisitiza.