Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 13,2022 visiwani Zanziabar wakati akitoa taarifa yake wiki kuhusu utekelezaji wa sera, miradi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akitoa taarifa yake wiki kuhusu utekelezaji wa sera, miradi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali leo Februari 13,2022 visiwani Zanziabar
…………………………………………………………
Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Zanzibar
Mwaka huu katika kuadhimisha miaka 58 ya Muungano wenye mafanikio makubwa na mfano wa kuigwa duniani Watanzania wameendelea kujivunia Muungano wao na tunu hiyo muhimu kwao.
Akizungumza leo Zanzibar, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa yake wiki kuhusu utekelezaji wa sera, miradi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali alisema kuwa licha ya kuwepo changamoto mbalimbali za Muungano Serikali hatukuishiwa maarifa na majawabu ya kukabiliana nazo.
Ambapo kumekuwepo na utaratibu wa kuwa na vikao vya pamoja vya kuzungumzia masuala ya Muungano ukiwemo utatuzi wa hoja za Muungano.
“Tulianza jukumu hili tangu mwaka 2006 tukiwa na hoja 25, tumefanya kazi kubwa ya kuzitafutia ufumbuzi, tukazipunguza hadi mwaka 2019 zikabaki hoja 18 na tarehe 24 Agosti mwaka jana 2021 tukaandika historia nyingine ya kuzifuta hoja 11 kati ya 18 katika vitabu vyetu kwa kuwa tayari zilikuwa zimeshapatiwa ufumbuzi” anasema Msigwa.
Alifafanua hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja na Muungano kuwa ni uingizaji wa maziwa Tanzania Bara kutoka Zanzibar. Ambapo waingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara walikuwa wanatozwa shilingi 2,000/- kwa lita, lakini sasa tozo hii imepunguzwa hadi shilingi 250/- kwa lita. Na waingizaji wa maziwa haya wamehimizwa kuzalisha maziwa kutoka Zanzibar badala ya kuingiza maziwa ya unga kutoka nje ya nchi na kisha kuyatengeneza kuwa ya maji na kuyaingiza Bara.
Hoja nyingine ni usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Msigwa aliendelea kufafanua hoja zingine zilizopatiwa ufumbuzi “Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Barabara ya Chake chake hadi Wete – Pemba, hoja hii ilitokana na kuwepo kwa sharti la lililotaka mkopo upatikane kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sharti hili liliondolewa” Alisisitiza Msigwa.
Hoja zingine ni Mkataba wa mkopo wa fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu.
Aidha, Ajira kwa Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano. Hoja hii imetatuliwa na Wazanzibar wanayo nafasi ya kuajiriwa Bara kupitia dirisha la ajira la sekretarieti ya ajira. Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Misaada kutoka Nje ya Nchi. Hivi sasa Zanzibar inatapa mgao na inaweza kuomba msaada kutoka nje ya nchi hata bila kibali cha Waziri wa Fedha na Mipango kama ilivyokuwa awali pamoja na Mapato yanayokusanywa na Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar. Hoja hii imeondolewa kwa sababu tayari maamuzi yamefanyika kwamba kila upande utakapokusanya mapato yatokanayo na visa yatabaki katika upande husika.
Sambamba na hayo, Msigwa alisisitiza kuwa Muungano ni imara na hivyo wanaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali hususani masuala ya maendeleo.
Baadhi ya masuala ya maendeleo wanayoshirikiana ni Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambao ulizinduliwa mwezi Februari, 2020 ambapo jumla ya shilingi bilioni 112.9 zinatumika Zanzibar na kazi inaendelea.
Fedha za Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na fedha hizo hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Majimbo. Kwa Majimbo ya Zanzibar kila mwaka hupokea shilingi bilioni 1.4 ambazo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Majimbo 50 yaliyopo Zanzibar.
Pamoja na mradi wa usogezaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo yana mawasiliano hafifu au hayana mawasiliano kabisa. Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Universal Communications Service Access Fund – UCSAF) na Kampuni ya Mawasiliano Zanzibar (Zantel) wameingia makubaliano mwezi Januari, 2022 ya kujenga minara ya simu 42 katika shehia 38 kwa lengo la kuboresha huduma ya mawasiliano Zanzibar. Mradi huu ukikamilika Zanzibar mtu atapiga simu akiwa mahali popote labda kutokee kikwazo maalumu.
Matokeo ya ushirikiano Matokeo wa Serikali hizi mbili yameleta mafanikio katika maeneo mbalimbali ambapo kuanzia mwezi wa Juni 2021 hadi sasa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu inayosimamia (DSFA) imekusanya Shilingi bilioni 2.4 na kutoa gawio kwa serikali (SMT na SMZ) ya asilimia 50 ya mapato hayoikilinganishwa na kushindwa kukusanya kabisa mwaka 2019 na 2020.
Mafanikio haya yametokana na kutungwa kwa sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu, Sura ya 388 ya mwaka 2020 ambayo imeridhiwa na Baraza la Wawakilishi. Kanuni zake zimeanza kutumika mwaka 2021. Sheria na Kanuni hizi zimechochea uwekezaji katika uvuvi wa Bahari Kuu.
Aidha, Kufadhili mradi wa Kutambua Maeneo yenye Samaki wengi Baharini (Potential Fishing Zone – PFZ). Jumla ya wavuvi wadogo 3,360 wamefaidika na mradi huu.