Mbunge wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela baada ya kufika kumpa pole kufuatia Kifo Cha mtoto wake, Dk Mwele Malecela.
…………………………………………………
MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa Mkoa huo amefika nyumbani kwa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela kumpa pole kwa msiba wa Mtoto wake, Dk Mwele Ntuli Malecela.
Ditopile amesema kifo cha Dk Mwele siyo tu pigo kwa familia yake bali ni pigo kwa Taifa na Afrika kwa ujumla kutokana na namna ambavyo ameitumikia Serikali na Mashirika ya kimataifa kwa kutanguliza maslahi ya wananchi.
” Nimefika kutoa pole kwa familia ya Waziri Mkuu Mstaafu Mzee wetu Malecela kwa msiba mzito wa Dk Mwele, hili siyo tu pigo kwa Taifa bali Afrika kwa ujumla kutokana na namna ambavyo Dk Mwele ameitumia taaluma yake kuwatumikia waafrika.
Kama Kiongozi nina wajibu wa kuyaenzi mazuri yote ambayo Dk Mwele ameyafanya enzi za Utumishi wake ndani ya Serikali yetu na Mashirika ya Kimataifa,” Amesema Mbunge Ditopile.
Dk Mwele amefariki Februari 10, mwaka huu jijini Geneva, Uswisi. Amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Ukurugenzi wa Taasisi ya Tafiti za Kiafya Tanzania (NIMRI) na baadaye Mkurugenzi wa Udhibiti wa Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele katika Shirika la Afya Duniani (WHO).