********************
12/02/2022 MOSHI, KILIMANJARO
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro hasa katika kipindi hiki ambacho ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi kuwasilisha kwake askari ambao wanafanya vitendo ya ovyo na visivyo na maslahi kwa taifa.
Waziri Masauni amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi katika shule ya Polisi Moshi Mkoani Kilimanjaro ambapo pia alimuagiza kamishna wa Polisi Zanzibar CP Awadh Juma Haji kwenda kuyashughulikia makosa ya udhalilishaji na dawa za kulevya.
Akifunga mafunzo hayo pia amewataka askari kuachana na vitendo vya kubambikia kesi na matendo mengine ambayo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro amesema zipo changamoto kama uhalifu unaovuka mipaka, ugaidi na na makosa ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine ya ulinzi na usalama vimeendelea kudhibitiwa licha ya kwamba bado zipo changamoto nyingine ikiwemo mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro SACP Ramadhani Mungi amesema jumla ya wanafunzi 1955 wamehitimu mafunzo ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi na kwamba wahitimu hao wamejifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na makosa ya uhalifu na wahalifu.