Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akimkabidhi Mkurugenzi wa Victoria Foundation Vicky Kamata taulo za Kike kwa ajili ya kuwasaidia mabinti wa kike waliopo shuleni ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo kipindi cha hedhi jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma kitaaluma.Baadhi ya Taulo za Kike ambazo zimetolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kw Taasisi ya Victoria Foundation ambazo zitatolewa kwa watoto wa kike waliopo shuleni kupitia kampeni ya Binti Ng’ara timiza malengo, inayowasaidia mabinti wanaokosa taulo za kike na kuwafanya kushindwa kuhudhuria masomo yao.
************************
Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa msaada wa taulo za kike paketi 1000 kwa Shirika lisilo la Kiserikali la Victoria Foundation kwa ajili ya watoto wa kike waliopo shuleni, ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kushindwa kuhudhuria masomo kipindi cha hedhi jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma kitaaluma.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi wa Shirila hilo katika Ofisi ndogo za Wizara ya Afya zilizopo jijini Dar es salaam Waziri Ummy amesema amepata msukumo wa kutoa taulo hizo ili kuunga mkono kampeni ya “Binti Ng’ara, Timiza Malengo” inayotekelezwa na Victoria Foundation kwa ajili ya kuwasaidia mabinti wanaokosa uwezo wa kununua taulo hizo.
Waziri Ummy amesema kampeni ya Binti Ng’ara ni kampeni nzuri kwani imelenga kumuinua mtoto wa kike ambaye alikuwa anakosa taulo inayomwezesha kujistiri pindi anapokuwa kwenye siku zake.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Victoria Foundation Bi. Vicky Kamata ameshukuru kwa msaada huo kutoka kwa Waziri Ummy na kusema utakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wakishindwa kuhudhuria masomo yao kutokana na kuwa kwenye hedhi na hivyo kusubiri mpaka wamalize ndiyo waendelee na masomo.
Kamata ametoa ombi kwa wadau wengine kujitokeza katika kuchangia kampeni hiyo, ili kuweza kuwasaidia mabinti hao wanaokosa masomo pindi wanapokuwa kwenye hedhi, na kuweza kuwasaidia kuondokana na changamoto hiyo.