Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiongoza kikao cha Menejimenti ya Wizara ya Maji cha mazungumzo na Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) akiwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (mwishoni kushoto) katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA), Sylvain Tusanga akizungumza katika kikao na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na Menejimenti ya Wizara ya Maji, katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko katika kikao cha mazungumzo na Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akipokea zawadi ya notebooks za Taasisi ya LTA kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA), Sylvain Tusanga mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko, Menejimenti ya Wizara ya Maji na Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA)mara baada ya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
……………………………………………………….
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ameongoza Menejimenti ya Wizara ya Maji kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) yenye Makao Makuu Jijini Bujumbura, Burundi katika ukumbi wa Wizara ya Maji Mtumba, Jijini Dodoma.
Ujumbe wa Sekretariati ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LTA, Bw. Sylvain Tusanga akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko umefanya mazungumzo na Waziri Aweso kwa lengo la kuelezea hatua zilizofikiwa katika utayarishaji wa utekelezaji wa mpango unaojulikana kama Lake Tanganyika Integrated Regional Development Programme (PRODAP) Awamu ya Pili, baada ya Awamu ya Kwanza ya mradi huo, unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, kukamilika kwa mafanikio.
Katika majadiliano, Mhe. Waziri wa Maji, amesisitiza kuwa LTA iwe suluhu ya matatizo ya maji kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, akisema kuwa wananchi wengi katika maeneo ya pembezoni mwa ziwa hilo hawana huduma za majisafi na salama na pia hawana huduma za usafi wa mazingira na kusababisha uchafuzi wa rasilimali za maji katika ziwa hilo.
Hivyo, kusisitiza kuwa LTA ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kuwa inatoa mchango stahiki katika kutatua kero hiyo kwa wananchi wa nchi zote nne (4) kwani changamoto wanazokumbana nazo wananchi waishio upande wa Tanzania ndizo wanazokumbana nazo wananchi katika nchi zingine wanachama wa LTA.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji, Sylvain Tusanga wa LTA ameiomba Wizara ya Maji kuwasilisha vipaumbele vyake ili viweze kuzingatiwa wakati huu wa maandalizi ya Awamu ya Pili ya Mradi wa PRODAP.
Bw. Tusanga ameelezea mradi mwingine unaotekelezwa na LTA unaojulikana kama Lake Tanganyika Water Management (LATAWAMA) unaohusisha na kuhakikisha kwamba rasilimali za maji zinasimamiwa na kutumika kwa uendelevu pamoja na kuzuia uchafuzi wa rasilimali hizo.
Sekretariati ya Bonde la Ziwa Tanganyika ndio chombo kinachosimamia shughuli za kila siku za Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika (Convention on Sustainable Management of Lake Tanganyika) ambao uliwekwa saini na nchi wanachama za Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia tarehe 12 Juni 2003 Jijini Dar es Salaam.