*************************
Na Lucas Raphael,Tabora
Walimu wakuu wa shule zote za msingi wilayani Nzega mkoani Tabora wametakiwa kutunza mazingira ya shule , kwa kuwa na shamba la mfano kwa kupanda miti ya matunda kwa lengo la kuboresha lishe ya watoto mashuleni.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa wilaya ya Nzega Acp Advera Bulimba ,ambaye aliwakilishwa na katibu Tawala wa wilaya hiyo Onesmo Kisoka wakati wa zoezi la upandaji wa miti 1500 lililofanyika kwenye shule ya msingi wita iliyopo katika kijiji cha wita kata ya ndala Tarafa ya Puge wilaya ya Nzega mkoani hapa
Alisema kuwa shule zote katika wilaya hiyo zinatakiwa kuwa na shamba la mfano ambalo litapandwa miti mbalimbali ya matunda ili kuongeza lishe kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule hizo.
Kisoka aliendelea kusema kwamba wilaya ya nzega ni miongoni mwa wilaya ambazo mazingira yake yameharibika kutokana na ukataji wa miti onvyo hivyo hakuna budi kutumia njia hiyo kupanda miti ya Matunda ,Mbao na ile ya Vivuli .
“Upandaji wa miti tofauti tofauti kutasaidia sana kuimarisha mazingira yetu na kuongeza wingi wa mvua ambazo zimekuwa zikinyesha chini ya wastani kila msimu wa masika unapoanza ‘alisema Kisoka.
Hata hivyo aliwataka walimu na wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi watoto na jamii kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza hasa kwenye mazingira tunayoishi.
Aidha alilishukuru shirika hilo la Kiraia la World vision Clasta ya nzega mkoani Hapa kwa kutoa miti kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi kuwa na utamaduni wa kupanda miti kwenye maeneo yanayozunguka shule hizo .
Awali mratibu wa mpango wa maendeleo ya Jamii wa shirika la World Vision Tanzania, Michael Ngasa alisema kwamba Asasi hiyo imetoa miti 1500 ambayo itapandwa katika shule za msingi nne na kituo kimoja cha Afya Busondo.
Alisema shule zitakazonufaika na mradi huo wa upandaji wa miti ya matunda na miti mingine ni shule ya msingi Izinga , Upungu, Wita,Kipungu na Kituo hicho cha afya.
Ngasa alitaja miti hiyo kuwa miti ya matunda 600,ambayo inajumuisha Michungwa ,Miembi aina ya Dodo ,Bolibo na Apple ,Miti ya vivuli 400 na Miti ya mbao 500
“Kuanzishwa kwa shamba hilo la mfano katika shule ya msingi Wita miti yote iliyopandwa itatunzwa vizuri ikue na kuleta kutimia kwa matarajio yetu”alisema Ngasa
Hata hivyo alizitaka Taasisi zingine ziunge mkono jitiada ya serikali ya wilaya kwa jamii hasa katika halmashauri ya nzega kupanda na kulinda na kuhifadhi miti kwa uboreshaji wa Afya na kipato cha kaya.