Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda ambaye pia ni Mlezi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT),akizungumza wakati wa kongamano hilo la vijana na Ibada ya Kitaifa ya Maombi iliyofanyika leo Februari 11, 2022 Jijini Dodoma.
Mwanzilishi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT), Bw. Isaac Mpatwa akieleza jambo wakati wa kongamano hilo la vijana na Ibada ya Kitaifa ya Maombi iliyofanyika leo Februari 11, 2022 Jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki katika kongamano hilo wakisikiliza mada mbalimbali
…………………………………………………………
Na.Mwandishi Wetu,DODOMA
WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ambaye pia ni Mlezi wa Taasisi ya KLNT,amewahimiza viongozi wa Dini nchini kuwaandaa vijana katika maadili bora ili waje kuwa viongozi bora na imara katika kulitumikia Taifa.
Mhe.Pinda ameyasema hayo leo Februari 11,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na vijana katika Kongamano la Uongozi wa Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) kuelekea maadhimisho ya siku ya National Breakfast Prayer yatakayofanyika.
Pinda amesema kongamano hilo litasaidia kuwatia moyo vijana kwa kuwahamasisha wapate matumaini ya kufanya mambo mengi ya kuchangia taifa.
“Kilichonivutia kwenye kongamano la mwaka huu ni mada ya uongozi kwa vijana na hili ni jambo la msingi kwa maana leo wanaonekana ni vijana, lakini kesho ndio viongozi,”.amesema
Pinda ameeleza kuwa uongozi lazima uendane na kumcha Mungu kwakuwa yeye ndiye muweza yote hapa Duniani hivyo mtu anapofanya jambo lake lazima amshirikishe Mungu.
“Wakati mwingine elimu isitutoe katika jambo hili la msingi kwa maisha ya binadamu maana Mungu ametupa akili lakini anajua vilevile kwamba unatambua yeye ndio mpaji wa hiyo akili,”amesema
Aidha Pinda amesema wengi waliopo sasa ni vijana wenye nguvu ya kufanya kazi hivyo watambue kuwa wapo kama vijana na kwa sasa lakini baadae watakuwa viongozi.
“Kumekuwa na utamaduni kwamba mtu akisoma kidogo au kuwa mwanasayansi wanajifanya wanajua zaidi kuliko Mungu, lakini mara wakipata ajali Mungu anatajwa kwanza, hivyo wanatakiwa kumtegemea Mungu”amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwanzilishi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT), Isaac Mpatwa amesema maandalizi yamekamilika ya mkutano wa tano unaoitwa Tanzania National Prayer Breakfast Youth Leadership Forum.
“Tayari mialiko mbalimbali kwa viongozi wa mihimili yote mitatu, wanafunzi, wafanyabiashara na kuhakikisha wanashiriki katika mkutano huo ambao utatanguliwa na mada mbalimbali kuhusu Utawala bora, uongozi na maadili ,”amesema