**************
NA GODFREY NNKO
KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala ameitisha maombi ya siku 121 kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kutokomeza roho ya mauaji ambayo imekuwa ikishamiri kwa kasi nchini.
Nabii Dkt.Joshua ameyasema hayo leo Februari 11, 2022 makao makuu ya Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania yaliyopo Yespa, Kihonda mjini Morogoro wakati akitoa taarifa rasmi ya ujumbe ambao amepewa na Mungu katika Taifa letu kuhusu mauaji ambayo yanaendelea kwenye Taifa letu tangu Januari hadi Februari, 2022.
“Huu ni ujumbe ambao Mungu amenipa kwa ajili ya kuliponya Taifa letu na kuliokoa dhidi ya mauaji ambayo yametikisa nchini, na yamekuja kwa tabia ambayo haijazoeleka katika jamii na nchi yetu, Mungu amenionesha kwamba, katika ulimwengu wa roho, ibilisi tayari ameweka ajenda yake ndani ya nchi yetu.
“Na anapelekea kusambaza roho ya mauaji ambayo baadaye itakuja kuingia katika ajenda za kisiasa. Lakini asili yake itaanzia kwenye makundi fulani ya kijamii. Kuna kabila kubwa katika nchi yetu, ambalo mimi ninasema ni kundi fulani katika la kijamii, litapandikiziwa roho ya chuki binafsi dhidi ya Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na wanasiasa watakapogundua hicho kitu watatumia hiyo nafasi kujenga chuki dhidi ya Serikali kwa ajili ya Uchaguzi wa mwaka 2025.
“Kwa hiyo, hiyo roho itasambaa, watu wataanza kulipa visasi na kuleta vurugu itakayosababisha mauaji makubwa sana 2025 ili kutia dosari katika uongozi wa Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan. Hii inawezekana, kwa sababu Biblia inasema kisha shetani akamuingia Yuda, halafu Yuda akapata tamaa ya kumsaliti Yesu ili auawe,”amesema.
Nabii Dkt. Joshua amesema kuwa,Yuda hakuwa hivyo asili yake, lakini shetani alimuingia,halafu alivyomuingia Mafarisayo waliokuwa wanamchukia Bwana Yesu,wakamtumia Yuda kumsaliti, akasaliti ili wampate kwa sababu wasingempata bila msaliti wake.
“Kwa hiyo katika ulimwengu wa roho hii nguvu itaendelea na watatokea watu ambao wanaaminiwa zaidi na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, watamsaliti.
“Kwa hiyo mifumo ya kiusalama na siasa za nchi zitavurugika kwa wakati huo na watu wabaya watatumiwa sana na ibilisi, kwa sababu ibilisi sasa hivi anatafuta watu wa kuwaingia ambao wana ushawishi katika nchi. Ikishaingia hiyo roho, itajenga sasa mpasuko ambao utatengeneza chuki, vikundi vya uhalifu vitaungwa mkono kufanya mauaji makubwa kwa ajili ya kuua ndoto za Mheshimiwa Rais Samia,”amesema.
Kwa mujibu wa Biliblia takatifu kitabu cha Mathayo 26:14-27:38, Nabii Dkt.Joshua alinukuu maandiko akionesha namna amabvyo Yuda alikubali kumsaliti Yesu.
“Kisha mmojawapo wa wale wanafunzi kumi na wawili aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa kuhani mkuu akamwambia. Mtanilipa kiasi gani nikimtoa kwenu? Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti Yesu.
“Siku ya kwanza ya sikukuu ya Mikate isiotiwa chachu wale wanafunzi walikuja kwa Yesu wakamwuliza? Ungependa tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?. Akajibu, nendeni kwa mtu fulani huko mjini mkamwambie, Bwana anasema hivi, saa yangu imekaribia, napenda kula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu nyumbani kwako.
“Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaambia, wakaandaa Pasaka. Ilipofika jioni, Yesu aliketi mezani pamoja na wanafunzi wake. Walipokuwa wakila akawaambia. Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti.Wakasikitika sana, wakaanza kumuuliza mmoja mmoja. Ni mimi, Bwana? Yesu akawaambia, yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami, ndiye atakayenisaliti.
“Mimi Mwana wa Adamu sina budi kufa kama ilivyoandikwa katika maandiko, lakini ole wake mtu yule atakayenisaliti. Ingalikuwa nafuu kwake kama hakuzaliwa. Kisha Yuda, yule ambaye alimsaliti akasema, “Ni mimi, Bwana? Yesu akamjibu,umetamka mwenyewe. Bwana? Yesu akamjibu, umetamka mwenyewe.
“Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, chukueni mle, huu ni mwili wangu.Kisha akachukua kikombe, akashukuru, akawapa akisema. Kunyweni nyote katika kikombe hiki. Hii ni damu yangu ya agano ambayo inamwagika kwa ajili ya wengi ili wasamehewe dhambi.
“Ninawahakikishia kuwa sitakunywa tena maji ya mzabibu mpaka siku nitakapoyanywa pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu. Walipokwisha kuimba wimbo walikwenda kwenye mlima wa Mizeituni. Kisha Yesu akawaambia, Usiku wa leo kila mmoja wenu atanikimbia kwa maana maandiko yanasema, nitampiga mchungaji, na kondoo wote wa kundi lake watatawanyika.Lakini baada ya kufufuka, nitawatangulia kwenda Galilaya.
“Petro akasema, hata kama wote watakuacha, mimi sitaku acha. Yesu akamjibu,ninakuambia kweli, usiku huu huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu. Lakini Petro akasema,hata kama itabidi nife pamoja na wewe, sitakukana. Na wana funzi wote wakasema hivyo hivyo.
“Kisha Yesu akaenda nao mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane. Akawaambia, kaeni hapa, mimi ninakwenda mbele zaidi kuomba.Akamchukua Petro, pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kufadhaika na kuhuzunika.Kisha Yesu akawaambia,moyo wangu umejaa majonzi karibu ya kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami,”amefafanua Nabii Dkt. Joshua kwa kunukuu maandiko matakatifu.
Pongezi
Aidha,Nabii Dkt.Joshua amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhadisi Hamad Masauni kwa kazi nzuri ambayo anafanya, ingawa amesema juhudi zake zinatatizwa kwa kukosa watu sahihi.
“Ni kweli vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kubwa sana. Hasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mhandisi Hamad Masauni) tumemuona anawajibika sana,na kwa kweli Mungu ambariki na Mungu ambariki Mama kwa kuona kuwa anaweza kumsaidia.
“Lakini amekosa watu sahihi, wa kumtia moyo na kumuunga mkono katika kazi anayoifanya. Jukumu letu sasa, mimi kama Nabii, Mungu ameniambia kuwa, nichukue hatua ya kulitahadharisha Taifa, kwanza viongozi wenye dhamana waanze kumtafuta Mungu kila mtu binafsi kwenye dhamiri yake, kwa sababu mamlaka hizi zinawekwa na Mungu,”ameongeza Nabii Dkt.Joshua.
Amefafanua kuwa, “Daudi alipoona hali mbaya ya Kitaifa alimlilia Mungu na Mungu alilipona nchi yake, kwa hiyo rai yangu ya kwanza ni viongozi wenye mamlaka kumlilia Mungu kwa sababu ni na hakika ni wazalendo. Na kazi kubwa ambayo mama yetu anafanya ni tishio kubwa kwa watu wengi ambao wana uchu wa madaraka.
“Kwa hiyo, sisi watumishi wa Mungu tutasimama, mimi binafsi na kanisa langu tumeitisha maombi ya siku 121 kwa ajili ya kutokomeza hii roho ili isistawi kwenye Taifa kiasi cha kuwafikia watu wabaya na kuwaletea maslahi maovu kwenye Taifa letu.
“Tunayo maombi ya siku 121 kwa ajili ya kumuinua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampiganie na kuweza kumpa nguvu na kuweza kutimiza majukumu yake, halafu pili Mungu aweze kumuondolea watu ambao si sahihi wanaomzunguka ambao wanasubiri siku moja wamsaliti. Na maombi yetu nina hakika kuwa yatafanikiwa.
“Lakini ni muhimu wajibu huu uwafikie viongozi wenye dhamana ya Taifa letu, kumtafuta Mungu kwa sababu nchi yetu imejengwa katika msingi wa bila dini, lakini katika hofu ya Mungu,”amesema Nabii Dkt. Joshua.