Mawaziri
wa Sekta ya Nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana leo tarehe 11
Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa 15 wa
Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya hiyo.
Mkutano
huu ulitanguliwa na mikutano ya awali ngazi ya Wataalamu/Maafisa waandamizi uliofanyika
tarehe 8 na 9 Februari 2022 na kufuatiwa na mkutano ngazi ya Makatibu Wakuu
uliofanyika tarehe 10 Februari 2022.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January
Makamba (Mb.) ambaye ameambatana na; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati – Tanzania
Bara, Mhandisi Felschesmi Mramba; Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini -Zanzibar;
Dkt. Mngereza Miraji; Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Petroli na Gesi kutoka
Wizara ya Nishati; Bw. Michael Mjinja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi
zake kwa ujumla.
Akihutubia
wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Makamba aliwakaribisha nchini wajumbe wa
mkutano huo na kuwahakikishia kuwa mkutano utafanikiwa kuyafikia malengo
yake kufuatia uongozi imara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe.
Peter Mathuki.
Vilevile
akaeleza ukanda wa Afrika Mashariki umejaaliwa rasilimali nishati za kutoka
hivyo, ni wakati sasa kwa kila nchi kuwa na mikakati imara ya kuhakikisha
nishati ya uhakika inapatikana ili kuihakikishia jamii upatikanaji wa huduma
zote zinazohitaji nishati.
“Tukiwa
tunapitia changamoto za ugonjwa wa COVID-19 tumeshuhudia namna gani nishati zilihitajika
katika kusaidia kuleta nafuu na kuokoa maisha ya wananchi wetu” alisema Mhe.
Makamba.
Naye
mwenyekiti wa mkutano huo na Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt.
Monica Juma alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watalamu na Makatibu Wakuu kwa
kufanya maandalizi mazuri ya Mkutano huo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa
umeme wa uhakika ni moja ya viashiria vya kukua kwa uchumi wa nchi yeyote.
Pia
akaeleza kukua kwa uchumi husaidia kupunguza utegemeze na hivyo jitihada za
makusudi zinahitajika kuziwesha Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya
uzalishaji wa kutosha viwandani na katika sekta ya kilimo.
Mkutano huu wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa
Kisekta la Nishati pamoja na mambo mengine utapitia na kutoa maamuzi juu ya;
Tarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa
hadi sasa katika sekta za Nishati Jadidifu, Nishati ya Umeme na Nishati ya
Mafuta; pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya
Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kadhalika mkutano huu utajadili kwa kina
utekelezaji wa mradi wa kituo cha Nishati Jadidifu cha Afrika Mashariki; Mradi
wa Kufua Umeme wa Nsongezi; Mradi wa kufua Umeme wa Murongo/Kigagati (14MW) na
Taasisi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati katika Nchi za Afrika Mashariki.
===================================================
Maafisa Waandamizi kutoka Wizara za Nishati Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. |
Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) |
Kutoka kushoto ni Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe pamoja na maafisa waandamizi kutoka Taasisi za Nishati wakifuatilia mkutano |
Ujumbe kutoka Kenya |
Ujumbe kutoka Uganda |