Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (wa pili kulia) akipokea kompyuta kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Sitholizwe Mdlalose (watatu kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya African Child Project , Catherine Kimambo ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mradi wa uunganishwaji wa shule kidigitali kwenye shule 50 za umma zilizoko katika mikoa 10 nchini(School Connectivity Project ), hafla ya makabidhiano imefanyika shule ya sekondari Mawenzi manispaa ya Moshi. Pichani kulia ni mwakilishi wa mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Arnold Msuya.
…………………………………………….
Moshi
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na taasisi ya African Child Projects (ACP) wamezindua rasmi upanuzi wa mradi wa uunganishwaji wa shule kidijitali kwenye shule ya sekondari ya Mawenzi iliyoko katika manispaa ya Moshi. Mradi unaolenga kuunganisha shule kadhaa nchini kwenye mtandao wa intaneti.
Chini ya makubaliano ya ushirikiano huu, taasisi ya ACP itatekeleza shughuli hizi katika shule 50 za umma zilizoko kwenye mikoa 10 nchini. Shule hizo zitapokea jumla ya kompyuta 186, tablet 246 pamoja na kupata vifurushi vya intaneti vya 50GB kila mwezi kwa mwaka mmoja.
Vodacom Tanzania Foundation ina historia ya kuwa na miradi ya elimu nchini Tanzania kwa miaka kadhaa sasa na imekuwa ikijitahidi kuleta mawazo bunifu kwenye suala zima la kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto na vijana katika jamii zenye uhitaji.
Akizungumzia faida za mradi huu, Sitholizwe Mdlalose, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc. alisema, “Ili kuweza kupambana na kuingia kwenye uchumi wa dunia, sisi ama nchi hatuwezi kukubali kuachwa nyuma, na hivyo basi tusikubali vijana wetu kukosa faida zinazotokana na mafunzo yanayotolewa kidijitali. Vodacom Tanzania tunaamini kuwa elimu bora ni msingi wa kujenga jamii ya kidijitali. Tunaelewa pia kuwa elimu bora ni jambo linalohitaji kufanyiwa kazi.”
Vodacom Tanzania imewekeza sana katika teknolojia na kupanua mtandao wake hadi kuwa shirika lenye mtandao mpana na wenye kasi kubwa kuliko mengine nchini.
Vodacom imejenga mfumo wa E-Fahamu na kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 hadi kufika mwaka jana, na kuwezesha wanafunzi 81,500 nchini kuweza kupata mafunzo bora na kwa kasi zaidi. Vile vile, mradi wa E-Fahamu, kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), umechangia kompyuta 1,400 na vifaa vya intaneti pamoja na kuunganisha shule za msingi na sekondari zilizoko kwenye maeneo ambayo yangeweza kusahaulika kwenye mtandao wa intaneti.
Mgeni rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Professor Adolf Mkenda alisema, “Tukiwa tunawajibika kwa utekelezaji wa sera za elimu, utafiti, huduma za Maktaba, Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na Uendelezaji wa Mafunzo ya Ufundi, tunahitajika kila siku kuwa makini katika kuona na kutambua njia bora za kutoa na kufikisha huduma hii muhimu kwa jamii zetu, haswa kwa wale walio maeneo ya mbali vijijini. Tunafurahia jitihada kama hizi zinazoendana na mkakati wa serikali wa kuharakisha upatikanaji wa maendeleo kwa wananchi.”
Ushirikiano huu na African Child Projects ulianza kwa mradi wa majaribio. Majaribio yalikamilishwa vema na ACP na wiki iliyopita mkataba mpya ulitiwa saini ili kupanua wigo wa mradi kufikia shule za Umma 50 zilizo katika mikoa 10 nchini.
Catherine Kimambo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya African Child Projects alisema, “Tunajivunia kuaminika kutekeleza mradi muhimu kama huu. Tunaahidi kuhakikisha tunautimiza kwa ubora mkubwa. Tunafanya hivi kwa sababu tunaamini kuwa elimu ni msingi ambao vijana tunaweza kujenga kutimiza ndoto zetu za maisha.”
Vodacom Tanzania inaamini kuwa mradi huu utachangia kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s), ambapo lengo namba tisa linalenga ‘kuongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za TEHAMA kwa gharama nafuu kwa nchi zinazoendelea’ pamoja na SDG 4 inayolenga, ‘Kuhakikisha usawa katika ubora na upatikanaji wa elimu ili kujenga mazingira endelevu ya kujifunza kwa wote.’