MAUAJI ya watu yanayotajwa kutokea maeneo mbalimbali nchini yanadaiwa kusababishwa na kukosekana kwa upendo,mshikamano na hofu ya Mungu miongoni mwa Watanzania na kuwataka kuonyesha mapenzi ya mfano wa njiwa (ndege) ili kukomesha vitendo hivyo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation,Khamis Mgeja alisema jana katika mazungumzo na waandishi wa habari kuhusiana na ongezeko la matukio ya mauaji ya watu hivi karibuni katika maeneo mengi hapa nchini.
Alisema kukosekana kwa upendo,mshikamano na hofu ya Mungu miongoni mwa jamii ya Watanzania ni moja ya vyanzo vya mauaji ya watu huku mauaji hayo yakihusishwa na kuwania mali (kugombea mali) na wivu wa mapenzi na ili kuepuka mauaji ya aina hiyo watu bila kujali itikadi za kiimani na makabila yao wamrejee Mungu .
“Ukichunguza kwa undani ni wazi mauaji hayo yanayoripotiwa maeneo mbalimbali nchini yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na watu kutokuwa na upendo miongoni mwao,watu kukosa hofu ya Mungu hasa ikizingatiwa wanaofanya mauaji hayo baadhi ni watu wa karibu ndani ya familia ambapo baadhi ya watoto wanawaua wazazi wao kwa lengo la kupata mali,”alisema Mgeja.
Mgeja alitoa mfano wake yeye mwenyewe amekuwa na tabia ya kuwakirimu njiwa (ndege) kwa kuwapa chakula na wao wameonesha upendo kwake ambapo kila siku asubuhi ndege hao hutua nyumbani kwake na kukaa naye ingawa wao si binadamu.
“Ukiacha wanadamu hata kama tutawakirimu viumbe wengine kwa kuwapa sadaka na kuwafanyia hisani, kuwahurumia na kuwathamini na wao pia wana nafasi kubwa ya kutuombea mbele ya muumba wetu ili tuishi kwa amani na upendo,” alisema Mgeja na kuongeza;
“Hali ya upendo ikidumishwa miongoni mwetu na kujenga utamaduni wa kuhurumiana sisi kwa sisi nchi yetu ama miji yetu itadumu kwenye amani na upendo, mfano ni hawa njiwa, mimi siwafugi,lakini huja hapa kila siku asubuhi, kisha wanaondoka, hii wanaonesha jinsi gani binadamu tunapaswa kupendana.”
Mwenyekiti huyo wa Tanzania Mzalendo Foundation,aliwaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini katika ibada na maombi yao ya kila siku wahimize sana suala la waumini wao kuwa na upendo na waone madhara ya kuuana wao kwa wao kwa mambo madogo madogo ya kidunia kwa vile duniani hapa ni mapito tu.
“Niwaombe Watanzania wenzangu,tumrejee muumba wetu bila kujali tofauti zetu za kidini,ukabila,kisiasa ama kijinsia, tukumbuke sisi sote ni ndugu, hatuna sababu za kuuana kwa suala la kutaka urithi ama wivu wa kimapenzi,tuisaidie serikali yetu kwa kuishi kwa amani na upendo ili tupate maendeleo,” alieleza Mgeja.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga na mwanasiasa mkongwe alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Watanzania kujenga utamaduni wa kupendana na kuhurumiana pale mmoja anapopatwa na matatizo asaidiwe badala ya kuchekwa,kama ni suala la mahusiano ya kimapenzi,busara itumike katika kutatua changamoto zinazojitokeza, badala ya kukimbilia kutoana roho.sss