Makatibu Wakuu wa sekta ya nishati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana leo tarehe 10 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania.
Mkutano wa Makatibu Wakuu ulitanguliwa na mkutano wa Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 8 na 9 Februari 2922. Mikutano hii mikutano ya awali kwaajili ya maandalizi ya Mkutano wa 15 Wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika kesho tarehe 11 Februari 2022.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Makatibu Wakuu umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ambaye ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Zanzibar, Dkt. Mngereza Miraji.
Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Makatibu Wakuu utapitia na kuandaa: Taarifa ya hali ya utekelezaji wa maagizo ya mikutano iliyopita; Hatua iliyofikiwa hadi sasa katika sekta za Nishati Umeme, Nishati Mafuta, na Nishati Jadidifu; pamoja na Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Kitaifa na Kikanda ya Sekta za Nishati inayotekelezwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Mwenyekiti wa Mkutano huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Maj. Gen. Dkt. Gordon Kihalangwa, CBS alieleza kuwa uhaba wa nishati ndani ya nchi zetu na jumuiya kwa ujumla huleta changamoto kwa wananchi wote na kushusha shughuli za uchumi na pato la taifa kwa ujumla. Hivyo, akasisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kutekeleza miradi ya nishati ya kitaifa na kikanda.
Vilevile akaeleza umuhimu wa sekta ya afya kupatiwa nishati ya kutosha na ya uhakika ili kuondoa changamoto za mara kwa mara zinazochangia kukosekana kwa huduma hizo.
“Huduma za mama na mtoto pamoja na huduma nyingine za afya ni muhimu zikazingatia upatikanaji wa nishati ili kupunguza matatizo yatokanayo na kukosekana kwa nishati ya uhakika kwa baadhi ya vifaa vinavyohitaji nishati ya umeme na gesi” alisema Dr. Gordon.
Mkutano huu umefanyika kwa njia ya mseto ambapo nchi za Tanzania, Kenya na Uganda wameshiriki mkutano wa ana kwa ana isipokuwa Burundi, Rwanda na Sudan Kusini wameshiriki kwa njia ya mtandao.
Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Nishati na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania Bara) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania Zanzibar), Dkt. Mngereza Miraji wakifuatilia majadiliano kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Mkutano huo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Jamhuri ya Kenya, Maj. Gen. Dkt. Gordon Kihalangwa, CBS (kati) akifungua Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 10 Februari 2022 jijini Arusha, Tanzania. Kushoto ni Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati waJamhuri ya Kenya, Mhandisi Benson Mwakina.
Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akifuatilia majadiliano katika mkutano huo.
Kutoka kushoto Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Mgeta Sabe na Mhandisi Emmanuel Yessaya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakifuatilia majadiliano.
Ujumbe wa Tanzania
Mkutano ukiendelea
Ujumbe kutoka Uganda
Ujumbe kutoka Kenya