Washabiki na wanachama wa Timu ya Yanga Tawi la Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakislisukuma Gari alilopanda Makamu Mwenyekiti wa Timu hiyo Frederick Mwakalebela alikwenda kufungua Tawi hilo jana.
Makamu Mwenyekiti wa Timu ya Yanga Frederick Mwakalebela aliyevaa fulani nyeusi na baadhi ya viongozi wa Timu hiyo Tawi la Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakikata utepe kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa tawi la Milonde.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Frederick Mwakalebela akiondoa kitambaa kwa ajili ya ufunguzi wa Tawi la Yanga Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,kushoto kwake Mwenyekiti wa Tawi John Stephano.
Baadhi ya wanachama na washabiki wa Timu ya Yanga tawi la Milonde wilayani Tunduru wakiwa katika Picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Timu hiyo Frederick Mwakalebela baada ya kufungua tawi hilo jana.
Baadhi ya viongozi wa Yanga Tawi la Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Timu hiyo Frederick Mwakalebela baada ya ufunguzi rasmi wa tawi la Yanga katika kijiji hicho.
…………………………………………………………..
Na Muhidin Amri,Tunduru
MAKAMU Mwenyekiti wa Timu ya Yanga Frederick Mwakalebela, amezindua Tawi la Yanga katika kijiji cha Milonde wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na kuwahaidi washabiki wa timu hiyo kuwa, msimu huu itakuchukua kombe la Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Hivyo, amewataka wanachama na washabiki wa Timu hiyo kuwa na furaha kwani viongozi wamejipanga kuhakikisha Timu hiyo hairudii makosa kama ilivyo fanya misimu minne iliyopita iliyosababisha kushindwa kuchukua kombe la Ligi Kuu.
Alisema,licha ya Ligi kuu ya mwaka huu kuwa ngumu kutokana na timu nyingi kujiandaa vizuri,lakini wana uhakika wa kuchukua kombe kutokana na usajiri wa wachezaji wenye uwezo mkubwa tofauti na misimu iliyopita.
Mwakalebela, amewaomba wanachama na washabiki wa Yanga kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika michezo ya Timu hiyo ili kuwapata nguvu wachezaji wao na wale watakaoshindwa kufika viwanjani waiombee dua ili ifanye vyema katika michezo yake.
Aidha alisema, wataangalia uwezekano wa Timu hiyo kucheza angalau mechi moja ya Ligi Kuu katika uwanja wa Majimaji ili kuwapa fursa wanachama,washabiki na wapenzi wa Timu hiyo waliopo mkoani Ruvuma wapate furaha na waishuhudie yao badala ya kuione kwenye Televisheni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Yanga Tawi la Milonde John Stephano alisema,kwa sasa Tawi hilo lina wanachama 105 kati yao wanaume 86 na wanawake 19,hata hivyo idadi hiyo itaongezeka kadri Timu hiyo itakapofanya vizuri katika michezo yake ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Alisema,lengo la kuanzishwa kwa Tawi hilo ni kuunganisha wanachama na washabiki wa Yanga kuwa kitu kimoja na kuimarisha Timu yao kiuchumi ili iweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Kwa mujibu wa Stephano tangu kuanzishwa kwa Tawi hilo kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya wanachama kutoka 56 hadi kufikia 105,kupata katiba mpya ya klabu na kusajili wanachama kwa njia ya mtandao.
Hata hivyo alisema, licha ya mafanikio hayo changamoto kubwa ni kukosekana kwa ofisi ya Tawi jambo linalo sababisha vikao na kazi za kiutendaji kufanyia kwenye nyumba za watu binafsi.
Alitaja changamoto nyingine ni kipato kidogo cha Wanachama hivyo kusababisha wanachama kusua sua kuchangia Timu yao na kushindwa kulipa ada kwa wakati.