Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akiwa kwenye mazungumzo na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati-Makete, Mchungaji Ezekiel Sanga, Katibu na Samwel Sanga, Mtunza Hazina katika ofisi za Wizara ya Maji, Mtumba, Jijini Dodoma.
Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati-Makete, Mchungaji Ezekiel Sanga, Katibu (kushoto) na Samwel Sanga, Mtunza Hazina katika ofisi za Wizara ya Maji, Mtumba, Jijini Dodoma.
Samwel Sanga, Mtunza Hazina wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati-Makete, mkoani Njombe akizungumza katika kikao na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Jijini Dodoma.
Kikao cha Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati-Makete, katika ofisi za Wizara ya Maji, Mtumba, Jijini Dodoma.
………………………………………………………………………
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali inathamini mchango wa Taasisi za Dini katika shughuli za maendeleo na itaendelea kuzipa ushirikiano wa dhati kwa manufaa ya taifa.
Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati- Makete, Mchungaji Ezekiel Sanga, Katibu na Samwel Sanga, Mtunza Hazina katika ofisi za Wizara ya Maji, Mtumba, Jijini Dodoma.
“Binafsi nathamini mchango wenu katika maendeleo ya nchi na Serikali inatambua kazi kubwa mnayoifanya kwa nia njema hususan kwenye Sekta ya Maji kwa ajili maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla ikiwemo kazi kubwa ya ujenzi wa miradi ya maji”, Katibu Mkuu Sanga amesema.
“Taasisi ya Dini kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 1.4 ni jambo kubwa sana, nikiwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji ninawashukuru sana kwa kujitolea kwenu na niwahakikishie ushirikiano wa dhati kutoka Wizara ya Maji wakati wowote”, Mhandisi Sanga amesisitiza.
Mchungaji Ezekiel Sanga, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Kusini Kati-Makete, amesema wameanza utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Lupombwe-Mbalache wenye thamani ya Sh. bilioni 1.4 katika Wilaya ya Makete, mkoani Njombe.
Amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 3,149 wa vijiji vya Lupombwe na Mbalache, akiongeza kuwa ujenzi wa chanzo umeshakamilika na wameanza kufanya utaratibu wa ununuzi wa mabomba.
Aidha, Mchungaji Sanga ameongeza kuwa wametekeleza jumla ya miradi 19 ya maji katika Kata za Lupila, Mbalache, Ipepo, Kipagalo, Bulongwa, Luwumbu, Tandala na Mang’oto.