*****************
Kampuni ya JATU PLC inayojishughulisha na Kilimo imemteua Msanii muziki Mrisho Mpoto “Mjomba” kuwa Balozi wa Kampuni hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ikiwa ni pamoja na kumwandalia kipindi maaluumu kitakachoitwa (kaa hapa Awamu ya pili ) kwaajili ya kuendelea kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa kutiliana saini na Msanii huyo Meneja Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC Mohamed Simbano amesema uamuzi huo umekuja mara baada ya Serikali February 7 mwaka huu,kumteua Mrisho Mpoto kuwa Balozi wa Maji kutokana na kutambua umuhimu wa Maji katika sekta ya Kilimo Jatu ikaona vema kuunga juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali.
“Kwetu sisi sekta ya Maji ni Moja ya Nguzo muhimu sana katika kuleta mapinduzi ya Kilimo,hasa kilimo cha Umwagiliaji ambacho tumekua tukifanya katika mikoa mbalimbali ndani ya miaka mitano toka kuasisiwa kwa kampuni ya JATU PLC kwakweli tunakila sababu ya kujivunia na kutembea kifua mbele tukiwa kama vijana tuliothubutu kwa kuishi ndoto zetu kwa kufanya kazi kwa vitendo na kisha kuaminiwa na kulelewa na serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano”amesema Simbano.
Aidha amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano JATU PLC imefanikiwa kuingiza kampuni katika soko la hisa la DSE, kufungua ofisi kikanda ndani ya nchi na afrika mashariki kwa kuanza na Kenya kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko ya ndani na nje,kufungua Kampuni ya Bima ya Kilimo na Ufugaji ,Ongezeko la Wakulima zaidi ya elfu tano,kutoa ajira rasmi miatano na zisizo rasmi zaidi ya elfu kumi,kuchochea maendeleo ya Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali.
Kwa upande wake Mrisho Mpoto “Mjomba” amesema Alisema kupitia fursa hiyo atatumia kutangaza mambo mazuri yanayofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan hususani Serikali imetilia mkazo katika sekta ya Maji,Mfano fedha za Uviko 19 serikali imetenga asilimia kumi ya fedha zote ambayo sawa na Bilion 139.8 na kupelekwa kwenye sekta ya Maji ambapo ndio sekta pekee iliyopewa fedha nyingi.
“najua watanzania wengi hawajui hilo lakini hiyo ni kazi yangu ya kuelimisha naenda kuifanya ” amesisitiza Mpoto.
“Serikali hii ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kupeleka maendeleo na kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa juu, mambo makubwa rais anafanya lakini hayasimuliwi mimi nitatangaza hayo mambo,” alisema mpoto
“Naishukuru Serikali tarehe 7 kuniteua kuwa balozi wa Sekta ya Maji,lakini baada ya hapo JATU leo tarehe tisa mkaniteua kwa mara nyingine kuwa balozi wenu kwa mkataba mkubwa wenye heshima kubwa, nawahidi sitawangusha,nitatumia kipindi cha Kaa Hapa awamu ya Pili kupitia Chaneli 10 siku Jumatano Saa nne Usiku,na Marudio yake Jumanne saa tano Usiku ili kutoa elimu kwa watanzania kujua umuhimu wa sekta ya Maji” amesema Mpoto
Mpoto aliteuliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuwa balozi wa sekta ya maji Februari 7, mwaka huu,hatua hiyo ilikuja muda mchache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kusifu umahiri wake wa kukariri gharama za miradi ya maji na kuzitamka, wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Bunda mkoani Mara.