p>
Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Alhajj Juma Killimbah ameongoza zoezi la uzinduzi wa kadi za Kielektroniki za chama hicho mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kadi hizo alisema CCM ni chama kikubwa ambacho hakiwezi kupitwa na chama chochote cha kisiasa hapa nchini na wakati wote kitaendelea kuwa mbele kutokana na mipango mizuri kiliyonayo.
Alisema uzinduzi unaofanyika leo ni muendelezo wa uzinduzi wa kitaifa uliofanyika wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya chama hicho uliofanyika mjini Musoma mkoani Mara ukiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.
“Tunachokifanya hivi sasa ni mabadiliko tunatoka kwenye mfumo wa kizamani wa analogia na kuingia kwenye mfumo wa kisasa wa kielekritoniki ambao utakisaidia chama chetu kupata Takwimu sahihi za Wanachama wake Kwa ngazi zote” alisema Killimbah.
Alisema chama hicho kinapotimiza miaka 45 tangu kuzaliwa kwake kimefanya mambo mengi ya kujivunia na sasa kimeingia kwenye mabadiliko haya makubwa ya kuwa na kadi za kielektoniki ambayo yanakwenda na kasi ya maendeleo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniphace alisema hadi sasa wanachama waliosajiliwa kielektroniki kwa mkoa mzima ni 69,437 na kuwa zoezi hilo linaendelea kwa wilaya zote.
“ Hadi sasa wanachama waliosajiliwa kwa mfumo wa Kielektroniki ni 69,437 Wilaya ya Iramba ikiongoza kuwa na wanachama 16,709 huku ikiwa na wanachama 54,982, ikifuatiwa na Singida Vijijini, 13,767 ikiwa na wanachama 47,071, Ikungi 11,329 ikiwa na wanachama 51,471, Manyoni, 10,592 ikiwa na wanachama 81,183, Singida Mjini 10,086 ikiwa na wanachama 33,843 na Mkalama 6,954 ikiwa na wanachama 56,140 huku jumla ya wanachama wote ikiwa ni 324,690.
Alitaja idadi ya kadi zilizopokelewa katika kila wilaya ni Iramba, 2663, Singida Vijijini 2638, Ikungi 361, Manyoni 2572, Singida Mjini 1831 na Mkalama 391 jumla zikiwa ni 10,456.
Aidha Boniphace aliagiza zoezi hilo la kusajili kieletroniki kasi yake iongezeke ili kila mwanachama ambaye hajapata kadi hiyo awe amepata kabla ya uchaguzi wa ndani ambao unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.