Washindi wa Tuzo za Dijitali Tanzania (Tanzania Digital Awards) 2021 wametangazwa rasmi baada ya mchakato wa kura kukamilika. Washiriki 57 kati ya 279 katika vipengele vikuu 12 na vipengele vidogo 53 wameibuka kuwa mabingwa wa kidijitali mwaka wa 2021. Washindi wamechaguliwa kutokana na mchango wao katika mageuzi ya kidijitali katika sekta zao na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Tanzania Digital Awards 2021 iliongeza vipengele vikuu vitatu zaidi na vipengele vidogo vinne kwa lengo la kutoa nafasi kwa wanamageuzi wengi zaidi wa kidigitali kushiriki. Vipengele vikuu kwa mwaka 2021 ni pamoja na Serikali Kidigitali, Diplomasia Kiditali, Masoko na Biashara Kidigitali, Burudani Kidigitali, Vyombo vya Habari Kidigitali, Ubunifu wa Kidigitali, Mawasiliano Kidigitali, Uchechemuzi Kidijitali, Benki Kidigiitali, Mawasiliano ya Simu Kidigitali, Tuzo ya Chaguo la Watu na Tuzo ya Heshima.
Diamond Platnumz kwa mwaka wa pili mfululizo ameibuka mshindi wa jumla kwa watu binafsi huku akinyakua tuzo mbili. Diamond ameshinda Tuzo za Mraghibishi wa Mwaka na Msanii Bora wa Kidijitali wa Mwaka (wa kiume).
Vodacom inaongoza miongoni mwa makampuni kunyakua tuzo zote nne katika kipengele cha Mawasiliano ya Simu Kidigitali. Vodacom imeshinda tuzo ya Kampuni Bora ya Mawasiliano ya Simu ya Mwaka, Kampuni ya Mawasiliano ya Simu yenye Huduma Bora kwa Wateja kwenye Mitandao ya Kijamii na Kampuni Bora ya Mawasiliano ya Simu katika Uvumbuzi. Pia, M-Pesa imepigiwa kura nyingi zaidi kama Aplikesheni Bora ya Huduma za Kifedha.
Benki ya CRDB imejinyakulia tuzo tatu, ikiwa ni pamoja na Benki Bora ya Mwaka, Benki Bora katika Uvumbuzi, huku Aplikesheni yake ya SIM Banking ikiibuka kuwa Aplikesheni Bora ya Huduma za Kibenki Kimtandao.
Idara ya Uhamiaji pia imeshinda Tuzo ya Taaisisi Bora ya Serikali Kidigitali kwa mwaka wa pili mfululizo. Taasisi nyingine za serikali ambazo zimeshinda tuzo mwaka 2021 ni Wizara ya Afya, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, na Mfumo wa Malipo wa Serikali (GePG).
Tuzo ya Mvumbuzi Bora wa mwaka imekwenda kwa Maarufu Muyaga wa Nderemo App. Tuzo ya chaguo la watu imekwenda kwa Jokate Mwegelo, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Kamati ya wataalamu imeimchagua ofisi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) kuwa mtunukiwa wa Tuzo ya Heshima kutokana na mchango wake katika kuchochea mapinduzi ya kidigitali nchini Tanzania. kusimamia utekelezaji wa malengo ya Ofisi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Ofisi ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ipo chini ya Shirika la Mawasiliano la Tanzania (TTCL).
TDA ilitangaza msimu wake wa pili mnamo Oktoba 2021, jumla ya majina 6800 ya watu binafsi na taasisi yalipendekezwa kuwania vipengele vikuu 12 vya tuzo, mapendekezo 279 yalipitishwa kwenda katika mchakato wa kura. Baada ya mchakato wa kura, timu ya wataalamu ilifanya tathmini ya kina na kuidhinisha majina ya washindi kwenye kila kipengele.
Vigezo vinavyotumiwa na kamati ya wataalamu ni pamoja na uvumbuni na usimamizi wa mabadiliko katika sekta husika, matokeo ya uvumbuzi husika katika jamii, matumizi bora ya teknolojia za kidigitali katika utoaji wa huduma, na mchango wa jumla katika mageuzi ya kidigitali.
Tazama orodha kamili ya washindi hapa? https://bit.ly/3rBVnQY.