*******************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MKUU wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Janeth Mayanja amesema vitambulisho vya Taifa 25,000 vimekwama kuchukuliwa na wananchi kwenye ofisi za kata na kutoa lawama kumbe hawajafuatilia wenyewe.
Mayanja ameyasema hayo akitoa maelekezo ya serikali, wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ kilichofanyika mji mdogo wa Katesh.
Amewaagiza madiwani hao kutoa taarifa kwa wananchi wao kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji, kata na Halmashauri ili kuwaondolea usumbufu wananchi wanaotembea umbali mrefu kwenda ofisi za mkuu wa wilaya kutoa malalamiko.
“Wananchi wengi wamekuwa wakija ofisini kwangu kulalamika kuwa hawajapata vitambulisho vya Taifa kumbe vipo ofisi za kata, inabidi tuwape taarifa wakavichukue ofisi za kata,” amesema Mayanja.
Amesema wananchi wengi wakiulizwa juu ya kuonyesha vitambulisho vya Taifa wanaonesha namba wakati tayari vitambulisho vyao viko ofisi za kata ila hawajavichukua.
“Mkiwa mnafanya vikao na mikutano yenu waambie wananchi kuwa vitambulisho vyao viko tayari wavifuate kwa maofisa watendaji wa kata,” amesema Mayanja.
Hata hivyo, Mkazi wa Katesh Nuru Luka akizungumzia kukosa vitambulisho vya Taifa amedai kuwa ukosefu huo unawakwamisha katika kupata mambo mbalimbali ya kijamii.
Mkazi wa mji mdogo wa Katesh Hawa Dayo amesema kitambulisho cha Taifa ni muhimu hakikwepeki kwani taasisi nyingi za umma zinahitaji ili kuweza kupata huduma tofauti.