Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma akizngumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Mafunzo kwa watoa huduma katika mnyororo wa utalii kupitia Mradi wa UVIKO -19 Awamu ya kwanza Mkoani Lindi.
Afisa Mtendaji Mkuu Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi akitoa
hotuba ya utangulizi wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yanayofanyika
katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Chuo cha Taifa cha
Utalii kimezindua rasmi mafunzo kwa watoa huduma katika Mnyororo wa Utalii
kupitia Mradi wa UVIKO 19 awamu ya kwanza kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali katika Mkoa wa Lindi.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa Mradi huo kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan
Ngoma ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi amesema kuwa Serikali
imeendelea kuchukua tahadhari katika mapambano dhidi ya janga la UVIKO -19 kwa kuweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha tahadhari zote muhimu zinachkuliwa.
Amesema kuwa katika
kipindi cha hivi karibuni kumeshuhudiwa jitihada kubwa iliyofikiwa na
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua kwa vitendo kwa kupeleka
fedha za Uviko -19 katika maeneo mbalimbali zikiwemo taasisi za Serikali ambapo
moja ya maeneo hayo ni Sekta ya Utalii na kwamba mafunzo hayo yatawawezesha wadau
wa Sekta hiyo kupata uelewa wa namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo wanapotoa
huduma zao kwa wageni.
Aidha ameongeza kuwa
kumekuwepo na shughuli nyingi zenye muingiliano wa wageni katika wilaya ya
Ruangwa kutokana na Wilaya hiyo kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo
ujenzi wa miundombinu na madini hivyo amepongeza Chuo cha Taifa cha Utalii
kuendesha mafunzo hayo katika Mkoa wa Lindi na kuweka kituo cha Mafunzo Wilayani
Ruangwa.
“Katika Mkoa wa
lindi hususani hapa Ruangwa kumekuwepo na shughuli nyingi za kiuchumi ukizingatia hii ni Wilaya inayoendelea
kutokana na shughuli zake zinazofanywa hapa ikiwemo Utalii na uchimbaji Madini
ambazo zimekuwa ikiwaleta watu wengi hapa wakiwemo wageni kutoka katika mataifa
ya nje” Amesema Ngoma.
Kwa upande wake Afisa
Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt. Shogo Mlozi amesema kuwa Mafunzo
hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ikiwa ni mafunzo
kwa watoa huduma kwenye Sekta ya Utalii na Ukarimu katika mikoa 8 ya Tanzania
Bara ikiwemo Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Iringa, Mwanza na
Mara, ambapo zaidi ya washiriki 150 watapatiwa mafunzo hayo kwa kila Mkoa
kulingana na ukubwa wa Mkoa na shghuli za Utalii.
“Sehemu ya pili ya
mafunzo haya, itahusisha utoaji wa mafunzo ya upimaji na upangaji ubora wa
madaraja kwa watoa huduma za malazi na chakula kwa jumla ya washiriki 47. Ambao kati
ya hao washiriki 14 wanatoka kwenye Sekta Binafsi na wengine watatoka katika
mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii” amesema
Dkt. Mlozi.
Aidha amewashukuru
washiriki wote kwa kukubali wito wa kuhudhuria mafunzo hayo kwani yatawajengea
uwezo wa kuinua ubora wa utoaji Huduma na ushindani katika Sekta ya Utalii.
Mafunzo hayo ya siku
tano yamezinduliwa rasmi leo Februari 7, 2022 katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani
Lindi na yanatarajiwa kufikia tamati Febrari 11 Mwaka huu.