***************************
Na. John Mapepele
Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Saidi Yakubu ameutaka uongozi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuifanya taasisi hiyo kuwa kituo chenye hadhi ya kimataifa kwenye utoaji wa taaluma ya Sanaa na utamaduni kuliko ilivyo sasa
Yakubu amesema hayo leo Februari 7, 2022 alipofanya ziara chuoni hapo na kuongea na watumishi na Menejimenti ya TaSUBa na baadaye kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo.
Amefafanua kuwa kutokana na upekee wa taaluma zinazotolewa na chuo hicho ambazo zinaendana na vyuo vya kimataifa hakuna sababu ya chuo hicho kubaki na hadhi yake ya sasa inayoongozwa na dira ya kutoa taaluma katika ubora kwa ngazi ya Afrika.
” Ni wazi kwamba kwa upekee wa chuo chetu na kozi zinazotolewa hapa ni lazima tuondokane na na fikra za Bagamoyo, Tanzania au hadhi ya Afrika na badala yake tuwe wa kimataifa ” ameongeza Yakubu.
Ameutaka uongozi kuwa mbunifu kwa kutumia raslimali za wizara mama kujitanua zaidi nchi nzima badala ya kufikiria eneo la Bagamoyo pekee.
Amekitaka chuo kuongeza udahili wa wanachuo ili hadhi ya chuo hicho iwe ya kimataifa ambapo amesisitiza kuwachukua pia wanafunzi kutoka nje ya Tanzania ili wawe mabalozi wa kukitangaza chuo katika nchi zao.