Na Godwin Myovela, Singida
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda amehimiza
watawa wote kuelekeza zaidi utume wao kwa kuhangaika na malezi ya watoto,
sambamba na kuzungumza na familia zinazowazunguka kama alivyohangaika Bikira
Maria na Yosefu kwa mtoto Yesu, ili kwa pamoja na umoja kutengeneza msingi
mzuri wa afya ya roho na mwili kwa ustawi wa maadili ya Taifa la Mungu.
Kuhusu mauaji yaliyojitokeza kwenye maeneo tofauti nchini,
hivi karibuni, sanjari na wimbi la biashara haramu za usafirishaji binadamu,
alisisitiza kuwa matendo hayo ni kiashiria cha kulega-lega kwa jukumu la kila
mmoja kwenye malezi na makuzi ya watoto ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu, hali ambayo hatimaye inazalisha matokeo hasi ya kimaadili ndani ya jamii.
Mhashamu Mapunda aliyasema hayo jana-jimboni hapa- kupitia
homilia yake kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya watawa wote waliowekwa wakfu
kwa Mungu, ambayo hufanyika kila Februari 2 ya kila mwaka kwa lengo la kuomba
na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya utume na utumishi wao.
“Tusijifungie tu ndani twende tukawashirikishe watu karama
zetu ili ziwaguse na kuwasaidia, tuwape faraja, upendo, tumaini, mwanga,
wokovu, tuzungumze na tuwe karibu na familia zinazotuzunguka kwa msaada wa sala
bila kuchoka kama walivyofanya Simeoni na Anna pale hekaluni, ili tuokoe jahazi
hili la kuporomoka kwa maadili, mauaji na biashara haramu za usafirishaji
binadamu,” alisema.
Aidha, kupitia homilia hiyo aliwatia moyo watawa hao kuongozwa
na maisha ya unyenyekevu, upendo, amani, uvumilivu, ushirikiano na kuishi kwa
fadhila ya usafi wa moyo kwa kuzingatia wote ni askari wa Kamanda mmoja-ambaye
ni Kristu-katika muktadha ule ule wa kumfanya apendwe na ajulikane ulimwenguni.
Mhashamu Mapunda pamoja na mambo mengine, aliwakumbusha
watawa hao wote wa kike na kiume kuguswa zaidi na maisha ya upendo sambamba na
kutoa ushuhuda wa imani, huku akimtaka kila mmoja kuwa zawadi kwa mwingine, jambo
ambalo litachagiza furaha na upendo miongoni mwao katika maisha yote ya utume
wao.
Alisema, Utukufu wa Mungu ni binadamu aliye hai hivyo kuna
kila sababu ya watawa hao kuendelea kuenzi na kuheshimu utu wa kila binadamu
bila ya kubagua wala upendeleo wakati wa kuwahudumia; ikizingatiwa kwamba utume
unaobagua watu sio utume wa Mungu, na binadamu wote ni mali ya Mungu na
wameumbwa kwa sura na mfano wake.
Katika hatua nyingine, aliwahimiza watawa hao kuhakikisha
ajenda ya utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yote yanayowazunguka inazingatiwa
na kupewa msukumo wa kipekee sababu kama mazingira yataharibika basi uhai wa
binadamu utapotea.
“Amecea (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Kanisa
Katoliki Afrika Mashariki na Kati) kwa mwaka huu, ambayo Tanzania ni mwenyeji, moja
ya ajenda yake ni mazingira…nawasihi sana watawa tujali, tuyatunze, tuyaenzi na
kuheshimu mazingira kama nyumba ya Mungu, na kwa kufanya hivyo tutakuwa
tunamtukuza Mungu;, kinyume chake tutakufa,” alisema Mhashamu Askofu Mapunda
Jimbo Katoliki Singida kwa sasa lipo kwenye maadhimisho ya
matukio mbalimbali kuelekea kilele cha Jubilei yake ya dhahabu ya miaka 50
tangu kuanzishwa kwake (1972-2022), ambapo pamoja na mambo mengine, imeelezwa
wakati huo jimbo likianzishwa kulikuwa na mashirika 6 pekee ya kitawa, na sasa idadi
yake ni zaidi ya 30.