Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akiongea na watumishi wa afya wa Mkoa wa Mara baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali yarufaa ya Mkoa.
Watumishi wa afya wa mkoa wa Mara wakimsikiliza Mganga Mkuu wa Mkoa
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akiongea na watumishi ambapo amewataka kuwashirikisha viongozi wa wananchi ili kuboresha huduma za afya.
…………………………………………………………
Na WAF- MARA
MGANGA MKUU wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amewaelekeza Wataalamu wa afya nchini katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali zote kuanzisha utaratibu wa kushirikisha viongozi wa kata na mtaa katika utoaji wa huduma ili kuondoa kero na malalamiko yanayotoka kwa wananchi.
Dkt. Sichalwe amesema hayo leo Februari 5, 2022 alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya na kuongea na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwl. Julius Nyerere Mkoani Mara.
Amesema, ili kuboresha utoaji huduma za afya kwa wananchi, ni muhimu kuwashirikisha wawakilishi wa wananchi viongozi wakiwemo Wabunge, Madiwani na viongozi wa kata vijiji/vitongoji ili kuibua kero na malalamiko ya wananchi, hali itayosaidia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
“Ni muhimu sana kuwamilikisha wananchi hospitali hizi ili kujua mahitaji yao, na hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko yanayoweza kuzuilika, mwisho kuboresha huduma kwa wananchi ” Amesema.
“Ukifuatilia mabadiliko ya utoaji huduma katika Sekta ya Afya nchini kabla na baada ya uhuru, utakiri kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika utoaji huduma na ubora za afya na kuboresha miundombinu ya majengo vifaa na vifaa tiba kwa kiasi kikubwa” Aliongeza.
Hata hivyo amesema Serikali imeweka alama kubwa katika Sekta ya afya kwa kujenga na kukarabati vituo vya afya vya kutosha, Hospitali za Rufaa za Mikoa, kanda, maalumu na Taifa, huku akisisitiza namna Serikali kupitia Wizara ya Afya inavyoendelea kuchukua hatua za kuboresha miundombinu, vifaa na vifaa tiba pamoja na kuendeleza watumishi katika taaluma zao.
Aidha, Dkt. Sichalwe amesema, Serikali imefanya makubwa sana katika upatikanaji wa ubora wa huduma kwa kusomesha wataalum katika ngazi za ubingwa na ubingwa bobezi na hivyo kufanya huduma bobezi kutolewa hapa hapa nchini tofauti na miaka ya nyuma.
Mbali na hayo Dkt. Sichalwe amesema, pamoja na uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya katika Sekta ya Afya nchini, bado Wananchi wanalalamika ubora wa huduma unatolewa
Hata hivyo, amewataka kuboresha usimamizi wa watarajali (intern) ili kuhakikisha wanapika/kuwaandaa vizuri wanafunzi wataokuja kuleta tija katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi hivyo amewataka wananchi kote nchini kushiriki katika miradi inayoendela na usimamizi wa rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Pamoja na hayo, Dkt. Sichalwe amewaagiza Watumishi wote katika Sekta ya Afya nchini kuweka kipaumbele katika utoaji elimu na uhamasishaji wananchi kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Pia Mganga Mkuu wa Serikali hakusita kuwakumbusha watoa huduma hao kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Shinikizo la damu, Saratani, Kisukani, na ajali za barabarani.“tuelimishe wananchi wetu wale chakula kama dawa ili huko mbeleni wasije kula dawa kama chakula kwa hivyo ni vyema kufishi mtindo bora wa maisha”.
Kwa upande wa tafiti aliwasisitiza wataalam hao kufanya hivyo ili kufuatilia mwendendo wa magonjwa yanayojitokeza kwenye jamii ili kusaidia kuboreshwa kwa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za afya
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Juma Mfanga amemshukuru Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe kwa kuongea na Watumishi ili kushirikiana katika kuboresha utoaji wa huduma hapa nchini
Pia, amemhakikishia Mganga Mkuu wa Serikali kuwa, kama msimamizi wa Sekta ya Afya ngazi ya Mkoa ataendelea kushirikiana na Wataalamu wengine ili kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19.