Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Injinia Mwanasha Tumbo akifungua mafunzo kwa watoa huduma za utalii kuhusu mwongozo wa kukabiliana na Janga la Uviko-19.
……………………………………………………………………………
Na Victor Masangu,Kibaha.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Injinia Mwanasha Tumbo amefungua rasmi mafunzo kwa watoa huduma za Utalii kuhusu Mwongozo wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Katika ufunguzi huo ambao ulihudhiliwa na watoa huduma kutoka wilaya mbali mbali za mkoa wa Pwani wakiwemo viongozi wa serikali pamoja na waalamu wa afya.
Mwanasha alimpongeza Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya dawa za chanjo kwa wananchi lengo ikiwa ni kupambana na maambukizi ya Uviko -19.
Pia alisema kuwa mafunzo hayo yataweza kuwajengea uwezo watoa huduma za utalii namna ya kukabiliana na UVIKO 19.
“Kwa kweli nawapongeza Sana kwa hatua hii ya Kuja katika Mkoa wa Pwani kuwapatia mafunzo haya ambayo nina imani yatawajengea uwezo kwa watoa huduma za utalii juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama.
Aidha aliwataka washiriki wote wa mkoa wa Pwani ambao wameweza kupata fursa ya mafunzo hayo kuyatumia vizuri na kuwataka wawe mabalozi wazuri katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupata chanjo.
“Kitu kikubwa ninachowaomba wale wote ambao tumeshiriki katika mafunzo haya inapaswa tumuunge mkono Rais wetu kwa vitendo kwa kuchanja ili wote tuweze kupata Kinga hii ambayo ni muhimu sana kwa afya yetu,”alisema Mwanasha.
Amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi msaidizi Idara ya utalii nchini Richie Wandwi amebainisha kuwa mafunzo hayo yatafanyika nchi nzima na kwamba yana umuhimu mkubwa katika kuendelea kuwajengea imani watalii na ulimwengu kwa ujumla.
Kadhalika alibainisha kuwa Tanzania imedhamiria kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kuweka mikakati kabambe ya kupambana na janga la UVIKO 19 kwa kutoa elimu pamoja na mafunzo mbali mbali kwa wananchi.
Piaamesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama.
“Kuwepo kwa changamoto ya Uviko- 19 kwa nchi yetu ya Tanzania kumeweza kupunguza idadi kubwa ya kuingia kwa watalii na kupelekea kushuka kwa uchumi na suala zima la kimaendeleo,”alisema Wandwi.
Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani Gunini Kamba amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika kupata chanjo ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo.
Kamba alisema kuwa katika Mkoa wa Pwani bado mwamko ni mdogo hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutimiza malengo ya serikali ya kila mwanachi apatiwe chanjo.
Mafunzo hayo yamehusisha watoa huduma mbalimbali kutoka Mkoa wa Pwani katika tasnia ya ukarimu na huduma za malazi na chakula kama vile katika hoteli, loji na kambi za kitalii; aina mbalimbali za waongoza watalii; watoa huduma katika shughuli za utalii wa kupanda mlima, uwindaji wa kitalii na utalii wa utamaduni; wakala wa safari za kitalii pamoja na wakala wa usafiri wa anga.