………………………………………….
Adeladius Makwega,WUSM.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ameileza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuwa Maoni na Maelekezo yote yaliyotolewa Februari 9, 2021 kwa wizara yake yamefanyiwa kazi.
Mhesmiwa Gekul aliyasema hayo Februari 4, 2022 mbele ya kamati hiyo chini ya Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Kirumbi Ngenda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini.
Mheshimiwa Gekul akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Said Yakub na wakurugenzi na wakuu kadhaa wa taasisi za wizara hiyo, alizitaja kanuni za Sheria za Filamu na Michezo ya Kuigiza zinazofanyiwa marekebisho ya 2022.
“Jina la kanuni, Kanuni inayobadilishwa, Marekebisho ya kanuni ya 5, Marekebisho ya Kanuni ya 8, Marekebisho ya kanuni ya 16, Marekebisho ya kanuni ya 23, Marekebisho ya kanuni ya 30, Marekebisho ya kanuni ya 34, Marekebisho ya ya jedwali 1 na marekebisho ya jedwali la 3.”
Aliyefungua kipenga cha kuchangia katika kamati hiyo alikuwa mjumbe Merdad Kalemani alisema kuwa ni vizuri marekebisho ya Kanuni na Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza yakachapishwa haraka katika gazeti ya serikali ili kuondoa zile kanuni ambazo zilionekana kuwa ni kero na hazina tija kwa sasa.
Mheshimniwa Kalemani akihitimisha mchango wake katika kamati hiyo alitoa pongezi kwa viongozi wapya wa wizara hii akiwemo Mheshimiwa Waziri Mohammed Mchengerwa na Naibu Katibu Mkuu Said Yakub.
Pongezi hizi pia ziliekezwa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuwateua watendaji wachapakazi, huku akisisitiza kuwa uteuzi huo unaongeza tija kubwa katika wizara zote.
“Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, ninashauri watendaji wapya wa wizara hii na wale wa zamani washirikiana na wafanye kazi vizuri, kama hivi alivyofanya Naibu Waziri Gekul mbele ya kamati yetu kwa kutuwasilishia vizuri, kwa umakini na uhodari.”
Akikiongoza kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimwa Ngenda, huku akitoa nafasi kwa wajumbe wake kutoa maoni na kuuliza maswali kwa ustadi mkubwa alilisitiza kuwa suala la tozo kwa kumbi la sinema liwe kwa kumbi zile zenye miundo mbinu tu.
“Nasisitiza hilo kwa kuwa wajumbe wangu kadhaa akiwemo mheshimiwa Polepole na mheshiwa Tarimo Wamelitaja hilo kwa kina, juu ya Vibanda Uumiza ambavyo vinaonesha mikanda kadhaa ya filamu kwa miaka mingi.”
Makamu Mwenyekiti Ngenda alifunga ukurasa wa kutoa maoni ya kamati hiyo kwa msisitizo kuwa sasa kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kufanya tafsri ya mikanda ya filamu kwa tafsri isiyo sahihi hivyo sasa ni wakati wa serikali kulitazama hilo kwa kina.