Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 31 wa Wakuu wa Nchi na Serikali Wanachama wa APRM kwa njia ya Mtandao akiwa ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Februari 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kutoa mchango wake kwenye Mpango wa Nchi za Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ili kuziwezesha nchi wanachama kujifunza kwake na yenyewe iweze kujifunza kutoka kwao.
“Tutaendelea kuungana na nchi wanachama kwenye mpango huu wa APRM ili tuweze kuwa sehemu ya mchango wa maendeleo ya nchi nyingine na sisi pia tuweze kujifunza kupitia nchi hizo katika maeneo ya kuimarisha demokrasia na utawala bora, usimamizi wa uchumi na maendeleo ya jamii.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 4, 2022) alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 31 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambao ni wanachama wa APRM uliofanyika kwa njia ya video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Mkutano huo uliongozwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Amesema kuwa mpango huo pia una utaratibu wa kufanya tafiti kwenye nchi wanachama kwa kushirikiana na taasisi za nchi husika kuona masuala mbalimbali ya kimaendeleo, changamoto na namna ya kuzikabili changamoto hizo.
Amesema kuwa mpango huo pia unatoa mafunzo kwa jamii kupitia makundi mbalimbali ikiwemo vijana, wabunge, asasi za kiraia, wanawake na watu wenye ulemavu na makundi mengine yanayoshiriki katika masuala ya demokrasia na utawala bora na sekta ya uchumi. “Tutaendelea kutoa mchango wa umoja wa Afrika na kuelezea mafanikio yetu na changamoto zetu katika umoja huo.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kupitia mpango huo, nchi wanachama zitaweza kupata mafanikio katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji, ujenzi wa viwanda, kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda, maliasili, uvuvi na madini. “Haya yote yanaangaliwa namna ambavyo nchi inaweza kujipanga katika kuinua uchumi wake.”
Amesema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya ripoti ya pili ambayo itawasilishwa kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama wa APRM. “Tanzania tunatarajia kupeleka taarifa kwa mara ya pili baada ya kupata tathmini ya nchi zote wanachama na sisi Tanzania kuona mafanikio tuliyoyapata na changamoto tulizozipitia.”
Katika mkutano huo ambao nchi za Namibia, Nigeria na Afrika Kusini ziliwasilisha ripoti za thamini za utendaji katika maeneo mahsusi kama lilivyo lengo la APRM, Burundi ilipokelewa kama mwanachama mpya na kufikisha nchi 42 zilizojiunga na mpango huo.
Katika mkutano huo, Rais Muhamad Buhari wa Nigeria amepitishwa kuwa mwenyekiti mpya wa APRM akichukua nafasi ya Rais Ramaphosa.