**************
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Bi. Mara Warwick katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Katika Mazungumzo yao Mhe. Ummy Mwalimu ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa maendeleo kwa Tanzania na kusaidia Sekta ya Afya nchini.
Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inatekeleza Mradi wa Investing in People (Kuwekeza kwa watu) wenye thamani ya zaidi ya Dola Milioni Mia Mbili za Kimarekani ambao unalenga kuboresha huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto nchini.
Waziri Ummy Mwalimu ameelekeza fedha za mradi huo zielekezwe kwenye kuboresha huduma za afya kwa kujenga miundombinu ya kutolea huduma kwa wajawazito, mama na watoto, kujenga wodi za watoto wachanga pamoja na kununua vifaatiba.
Kuhusu mapambano dhidi ya UVIKO-19 Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na shughuli ya utoaji wa chanjo nchini kote na kuikaribisha Benki ya Dunia kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel ameiomba Benki ya Dunia kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na chanjo nchini.
Mwakilisha Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Mara Warwick amepongeza juhudi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za afya nchini pamoja na mapambano dhidi ya UVIKO-19.