Mkurugenzi wa makumbusho ya Azimio la Arusha,Dokta Gwakisa Kamatula akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo kuhusu maadhimisho hayo.(Happy Lazaro)
………………………………………………………
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Wananchi jijini Arusha wametakiwa kutembelea makumbusho ya Azimio la Arusha ili kuweza kujua historia na kujifunza mambo mengi kuhusiana na nchi kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Dkt Gwakisa Kamatula Mkurugenzi wa makumbusho ya Azimio la Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Azimio la Arusha litakalofanyika febuari 4 mwaka huu.
Amesema kuwa ,watu wameanza kusahau misingi iliyowekwa na waasisi wa nchi akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hivyo mwaka huu wakaona wawe na wiki ya maadhimisho ambayo yameanza Februari 1 hadi 4.
“Lengo kubwa ni kujaribu kuwakumbusha watanzania kuhusu umuhimu wa misingi iliyowekwa katika Azimio la Arusha na watu wengi wanajiuliza kwanini imeitwa Azimio la Arusha lakini ni Azimio la Arusha kwa maana kwamba maazimio, maamuzi ya nchi kuhusiana na sera za kufuata hasa baada ya uhuru yalifanyika hapa,” amesema Dkt Gwakisa.
Amefafanua kuwa, ilibidi viongozi wakae waamue ni jinsi gani wataiendesha nchi, ni sera gani wataifuata na ni misingi gani waiweke ili viongozi wa nchi na wananchi kwa ujumla waifanye ili wote kwa ujumla waweze kwenda sawa hivyo kuwekwa misingi imara sana, misingi ya uongozi na misingi ya kulinda utaifa.
“Kwanza ni kulinda utaifa ambao nchi yetu ilikuwa imeshapata uhuru lakini kuhakikisha kwamba kuna kuwa na haki na usawa kwa wananchi wote lakini pia walisisitiza kuwa nchi yetu ni maskini inabidi kila mmoja wetu aweze kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo binafsi na kuiletea nchi maendeleo kwa ujumla wake,” amesema.
Amefafanua kuwa, ni sera ambazo zilisaidia kuifikisha nchi hapa ilipo ikiwemo vita dhidi ya Rushwa, vita dhidi ya uonevu, matabaka na mambo mengine mengi hivyo lengo la maadhimisho haya ni kuendelea kuwakumbusha wananchi Kuna umuhimu wa kulinda uzalendo, uwajibikaji na kuweka mbele utaifa kama ambavyo maazimio yalivyotarajiwa.
“Waje wauze kazi zao, wajitangaze, tunao wasomi wengi mtaani ambao badala ya kukaa tu na kusubiri ajira ya serikali waje wajifunze hapa tutakuwa na mada kutoka kwa wataalamu mbalimbali kuhusiana na suala zima la namna ya kufanya ujasiriamali, kujitegemea kiuchumi lakini pia tutakuwa na mtaalamu kutoka tume ya maadili ambaye atakuja kutukumbusha kuhusiana na suala la uzalendo , utaifa na maadili ya mtu mmoja mmoja na hata viongozi,” amesema Dkt Gwakisa.
Amesema kuwa,sambamba na maadhimisho hayo siku ya kilele wanatarajia kuzindua mradi wa kuboresha makumbusho ya Azimio la Arusha ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu wamewapatia fedha za kuweza kuifanya makumbusho hayo kuwa ya kisasa, kuweka maonesho ya kisasa, vifaa vya kiteknolojia yanayoendana na wakati ili wananchi au watalii wa ndani na nje watakao tembelea waweze kupata historia ya nchi kwa uzuri na kwa wepesi zaidi.